1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wachezaji wa Gladbach wapunguza mishahara kutokana na corona

Josephat Charo
20 Machi 2020

Borussia Moenchenglabach inayoshiriki ligi ya Bundesliga Alhamisi (19.03.2020) imekuwa klabu ya kwanza ya soka la kulipwa ambayo wachezaji wake wamekubali kwa hiari kukatwa mishahara kusaidia walioathirika na Corona

https://p.dw.com/p/3ZnyQ
Fussball, Bundesliga | Borussia Mönchengladbach - 1. FC Köln
Picha: picture-alliance/dpa/U. Hufnagel

Mkurugenzi wa michezo ndani ya klabu hiyo, Max Eberl, alisema kuwa timu ya kiufundi katika timu hiyo wamejiunga na mchakato huo wa kuchangia fedha kwa hiari ili kuwasaidia waathirika wa janga hilo kama walivyofanya wakurugenzi na uongozi wa juu wa klabu hiyo.

Kando na hilo, Jan-Christian Dreesen ambaye ni afisa mkuu wa fedha katika vigogo wa soka nchini Ujerumani, klabu ya Baryen Munich, alionya: "Kitu kimoja tayari kiko sawa katika soka la kitaifa na kimataifa, ligi za vilabu na vyama vya soka vinakabiliwa na changamoto kuungana pamoja."

Gladbach itaokoa zaidi ya euro milioni 1 sawa na dola za Kimarekani milioni 1.1 kwa mwezi, hii ni kwa mujibu wa gazeti la Rheinische Post la hapa Ujerumani.

Wachezaji pamoja na viongozi wengine wanaolipwa kiasi kikubwa cha fedha walitaka kulinda kazi na vipato vya watu wengine ndani ya klabu. "Ninajivunia vijana hawa," alisema Eberl. "Tumesimama pamoja kama Borussia katika nyakati za raha na shida. Walitaka kurejesha kitu fulani kama fadhila kwa Borussia na kwa mashabiki wote wanaotuunga mkono."


Kwa hivi sasa ligi kuu ya Ujerumani Bundesliga imeahirishwa angalau hadi Aprili 2 lakini wachache katika soka wanatarajia mara moja mambo yatarudi katika hali ya kawaida.

Klabu ya Karlsruhe inayoshiriki katika ligi ya daraja la pili hapa Ujerumani ilisema wachezaji wake watalipwa sehemu ya mshahara wao, huku timu ya Mainz iliyopo ligi kuu ya Bundesliga ikisema kuwa ajira katika klabu yake imebaki salama kwa muda mrefu.

Wachezaji wafutwa kazi Uswisi

Wakati hayo yakijiri, gazeti la Blick limeripoti kuwa klabu ya Sion iliyoko ligi kuu nchini Uswisi iliwaachisha kazi wachezaji wake kadhaa nyota. "Wote tumenyimwa mapato yetu," rais wa klabu hiyo Christian Constantine alinukuliwa akisema. "Haturuhusiwi mkataba wa kazi na hawaruhusiwi kufanya kazi," alisema kuhusiana na wachezaji wake.

Kulingana na gazeti hilo la Blick, Constantine alijaribu kupata wachezaji watakaokubali saa chache za kufanya kazi, lakini walikataa kusaini karatasi muhimu ndani ya tarehe ya mwisho aliyokuwa amewapatia wachezaji hao. Umoja wa wachezaji nchini Uswisi, SAFP, umetangaza kuwa utambania masilahi ya wachezaji hao.

Akizungumzia suala hilo, Dreesen ambaye ni afisa Mkuu wa fedha wa kigogo wa soka wa Bayern, alisema ama kwa hakika klabu yake imeweza kufanya vizuri katika miaka ya hivi karibuni hatua iliyoiwezesha klabu hiyo kuondokana na mtikisiko wa kiuchumi," lakini nakubali sina uhakika kama mapambano dhidi ya virusi vya Corona yataendelea.

"Hatuwezi kusema leo ni kwa muda gani mlipuko huu utakwisha na ni hatua gani zaidi zitakazochukuliwa pamoja na hatua zile zilizokwishachukuliwa kupambana na virusi hivyo hatari," alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa fedha wa klabu ya soka ya Gladbach, Stephan Schippers awali alisema kuwa kila mechi ya nyumbani ambayo milango ya uwanjani ilifungwa kama ile dabi ya hivi karibuni waliyoshinda dhidi ya Cologne, iliigharimu klabu karibu euro milioni 2.

Na kama msimu wa Bundesliga hautamalizika huenda kukatokea hasara kubwa hasa kutokana na mapato yatokanayo na matangazo ya televisheni.

"Malengo ni kwamba Borussia Moenchengladbach wananusurika kuanguka kiuchumi hasa kutokana na mlipuko huu wa virusi vya Corona," alisema Schippers." Lengo ni kwamba tunafanya hivi bila kuwa tufaa."

Mwandishi: Deo Kaji Makomba/dpa

Coronavirus - Köln
Nembo ya klabu ya FC Köln kwenye lango la kuingilia uwanjani baada ya ligi kuu ya Bundesliga kusitishwaPicha: picture-alliance/dpa/F. Gambarini

Mhariri: Josephat Charo