1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wade apinga vikwazo dhidi ya Mauritania

Kalyango Siraj23 Oktoba 2008

Je ni pigo kwa vita dhidi ya mapinduzi?

https://p.dw.com/p/FfH8
Rais Abdoulaye WadePicha: AP

Rais wa Senegal Abdoulaye Wade amesema hakubaliani na suala la kuiwekea vikwazo vya kimataifa nchi jirani ya Mauritania kama nji ya kuwabinya viongozi wa mapinduzi ya kijeshi ya ili kumrejesha madarakani kiongozi wa nchi hiyo aliechaguliwa kidemokrasia.

Rais Wade licha ya kutokubaliana na wazo la vikwazo hata hivyo, amewaambia waandishi habari kuwa haungi mkono hatua ya majenerali wa Mauritania katika kindendo chao.Wanajeshi wa Mauritania, Agosti 9 walimpindua rais Sidi Mohamed Ould Cheikh Abdallah, ambae sasa yuko kizuizini.Sasa nchi hiyo inaongozwa na Generali Mohamed Ould Abdel Aziz.

Kitendo cha wanajeshi kuupindua utawala uliochaguliwa kidemokrasia kilipingwa na jamii za kimataifa mkiwemo na Umoja wa Afrika ambao miongoni mwa mwingine ulitaka utawala wa sasa utengwe.

Wiki hii kiongozi wa kijeshi wa Mauritania alipinga miito kutoka kwa Umoja wa Ulaya pamoja na Umoja wa Afrika wa kutaka kurejeshwa madarakani kiongozi aliepinduliwa.Kiongozi wa kijeshi alisema kamwe hilo haliwezekani.

Generali Abdel Aziz,pamoja na washirika wake, wanamlaumu Cheikh Abdullahi, aliepinduliwa, kwa kushindwa kukabiliana na changamoto za kiuchumi na kiusalama,kama vile kupanda kwa bei ya vyakula na ya petroli na pia kushindwa kukabiliana vilivyo dhidi ya mashambulizi ya wanaharakati wa kundi la Al Qaida.Majenerali hao walichukua madaraka baada ya rais wa zamani kuamuru wafukuzwe kazi.

Wiki iliopita serikali ya Marekani iliwawekea baadhi ya viongozi wa serikali ya kijeshi vikwazo vya kusafiri kwenda nchini humo.Mapema wiki hii Umoja wa Ulaya uliupa muda wa mwezi mmoja, utawala wa kijeshi wa Mauritania, kumuachulia huru na kumrejesha madarakani kiongozi aliepinduliwa,la sivyo taifa hilo litawekewa vikwazo zaidi. Tayari Umoja huo umesitisha msaada wowote ambao si wa kibinadamu kwa Mauritania.

Rais Wade kwa upande wake anasema anapendelea usuluhishi badala ya vikwazo,akitoa hoja kuwa vikwazo kamwe haviwaumizi viongozi bali watu wa kawaida.Aidha amesema kuwa ni lazima kile alichoita 'ukweli' kifikiriwe kuhusu Mauritania. Amesema kuwa bunge la taifa pamoja na baraza la seneti baado vipo vikifanya kazi kama kawaida na wengi wa wajumbe wa mabaraza hayo waliunga mkono mapinduzi hayo.Kwa hivyo yeye msimamo wake unapinga vikwazo.

Msimamo huu wa rais Wade,ambae ana uhusiano mzuri na mataifa ya magharibi, ni kama pigo kwa hatua za Umoja wa Ulaya , Umoja wa Afrika pamoja na Marekani za kuzidisha mbinyo kwa watawala wa kijeshi waliochukua madaraka nchini Mauritania mwezi agosti mwaka huu kuachia madaraka.

Maandamano ya barabarani, ya hapa na pale nchini Mauritania kupinga mapinduzi hayo, yamekuwa yakivunjwa na vikosi vya vya usalama.