1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waganda wajiwekea akiba Kenya inapoingia katika uchaguzi

7 Agosti 2017

Baadhi ya wafanyabiashara wameelezea mashaka kuhusu uchaguzi nchini Kenya, wakisema ushindani mkali unaweza kuzusha machafuko. Kama tahadhari, wamenunua kiasi kikubwa cha bidhaa zinazoagizwa au zinazopitia Kenya.

https://p.dw.com/p/2hpJk
Insekten als Nahrung in Afrika
Picha: picture-alliance/dpa

Nchi Uganda, baadhi ya raia na hasa wafanyabiashara wameelezea mashaka kuhusu uchaguzi nchini Kenya, wakisema ushindani mkali kati ya wagombea urais wawili unaweza kuzusha machafuko iwapo upande utakaoshindwa utapinga matokeo. Kutokana na hofu hii wengi wamenunua kiasi kikubwa cha bidhaa zinazoagizwa kutoka au kupitia Kenya huku wengine wakizihodhi bidhaa hizo kufuatia ujumbe wa tahadhari unaosambazwa kwenye mitandoa ya kijamii.

Tangu machafuko yaliyozuka baada ya uchaguzi mkuu wa Kenya mwaka 2007, msimu wa uchaguzi katika taifa hilo jirani kwa upande wa mashariki huleta mashaka makubwa kwa wananchi wa Uganda hasa wafanyabiashara na wale walio na jamaa zao upande huo wa mpaka. Halima Abdalla ni mwanahabari ambaye amefuatilia maoni ya waganda kuhusu uchaguzi huo na anasema "Watu wanahofia huenda hali ikawa kama ile ya mwaka 2007 ambapo wafanyabiashara walipoteza bidhaa zao na bei ya mafuta ikapanda zaidi."

Sababu ya hofu ni gani?

Bildkombo Kandidaten Wahlen Kenia 2017

Safari hii hofu na mashaka kuhusu uchaguzi huo utakaofanyika hapo kesho ni kutokana na ushindani mkali uliodhihirika kupitia kwa taarifa za watabiri na jinsi kampeni hizo zilivyopamba moto. Vuta nikuvute kati ya familia mbili zenye jadi ya uhasimu wa kisiasa nchini Kenya inaleta tumbo joto kwa waganda. David Kageruka ambaye ni mfanyabiashara wa miaka mingi amesema "Kama wako bega kwa bega hali ya wasiwasi inakuwa juu zaidi kwa sababu ni rahisi mmoja kusema ameibiwa. Ingekuwa bora kama mmoja yuko juu zaidi ya mwenzake, basi hapo tusingekuwa na wasiwasi."

Hata hivyo maombi ya wengi nchini Uganda ni kwamba uchaguzi huo uwe wa amani na utulivu ili watu wa nchi hizo waendelea na shughuli zao za kawaida haraka iwezekanavyo. 

Lakini baadhi ya waganda haoni tatizo lolote na kuchukua tahadhari na ndiyo maana mijadala inayotawala kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii ni kwamba watu wahifadhi bidhaa muhimu kama mafuta ili waepushe shughuli zao kukwama licha ya makampuni husika kutoa hakikisho kwamba kuna kiasi cha kutosheleza kwa hadi wiki tatu.

Ikumbukwe kwamba hadi sasa kuna zaidi ya raia mia tatu wa Kenya ambao wangali Uganda kama wakimbizi kufuatia machafuko ya mwaka 2007.

Mwandishi: Lubega Emmanuel, DW - Kampala

Mhariri: Iddi Ssessanga