1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wagombea urais wa Democratic wakutana kwa mdahalo Marekani

Yusra Buwayhid
27 Juni 2019

Wagombea Urais kupitia chama cha Democratic nchini Marekani wamefanya mdahalo wao wa kwanza Jumatano ambao umezingatia masuala ya huduma ya afya, Iran pamoja na mabadiliko ya tabia nchi.

https://p.dw.com/p/3L9YX
TV-Debatte von zehn Präsidentschaftsbewerbern der US-Demokraten
Picha: picture-alliance/newscom/K. Dietsch

Wagombea wanaongoza katika kinyanga'nyiro cha urais ndani ya chama cha Democratic Jumatano walijadili masuala kadhaa ikiwa ni pamoja na huduma ya afya, sera za kigeni, ukatili unaotokana na umiliki wa silaha, na uhamiaji haramu, katika sehemu ya kwanza ya mdahalo huo wa siku mbili.

Seneta wa Marekani Elizabeth Warren, ambae ni miongoni mwa wagombea wanaoongoza katika kinyang'anyiro hicho amesema atapigania huduma ya afya inayofadhiliwa na serikali na kuwakosoa wale ambao wanapinga mfumo wa afya wa aina hiyo.

"Wanachokwambieni hasa ni kwamba hawataki kulipigania hilo," amesema Warren. "Huduma ya afya ni huduma ya msingi kwa binadamu na mimi nitapigania haki za msingi za binadamu. "

Suala la huduma ya afya limekuwa muhimu sana katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2020, hasa baada ya Rais Donald Trump kusaini amri ya kufuta sehemu ya mpango wa afya wa rais aliyemtangulia Barack Obama, uliokuwa ukijulikana maarufu kama Obamacare.

TV-Debatte von zehn Präsidentschaftsbewerbern der US-Demokraten
Elizabeth WarrenPicha: picture-alliance/newscom/K. Dietsch

Usalama wa nchi na mabadiliko ya tabia nchi

Kuhusu suala la Iran, Seneta wa jimbo la New Jersey Corey Booker ndiye mgombea pekee aliyesema haungi mkono makubaliano ya nyuklia na Iran na kwamba ulikuwa ni "uamuzi wenye makosa."

Suala la Iran limekuwa mjadala mkubwa miongoni mwa wapiga kura wa Marekani katika wakati ambapo nchi hiyo inavutana na Marekani kuhusu mashambulizi ya meli za kubebea mafuta yaliyotokea Ghuba ya Uajemi hivi karibuni. Lakini baadhi ya wagombea masuala mengine ya usalama waliyapa kipaombele zaidi.

Gavana wa jimbo la Washington Jay Inslee amesema amestaajabishwa sana kwamba suala la kupambana na mabadiliko ya tabia nchi halikupewa kipaumbele na wagombea wengi katika mdahalo huo.

Inslee amesema kizazi cha le ndiyo cha kwanza kushuhudia uchungu wa athari za mabadiliko ya tabia nchi na ndiyo cha mwisho kinachojaribu kupambana na hali hiyo.

Makamu wa zamani wa rais Joe Biden na Seneta Bernie Sanders, ambao wanaongoza katika utafiti wa maoni ya wapiga kura, watapambana katika sehemu ya pili ya mdahalo huo Alhamisi jioni.