1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waguzi watano wa Ki-Bulgaria na daktari wa Kipalastina wameondoka Libya

24 Julai 2007

Wamesharejea nyumbani. Nakusudia wauguzi watano wa Ki-Bulgaria na daktari mmoja, ambao walihukumiwa nchini Libya, wamondoka nchini humo. Huko Libya walishtakiwa kwamba, kwa makusudi, waliwaambukiza watoto wa Ki-Libya na virusi vya UKIMWI.

https://p.dw.com/p/CHAd
Wauguzi watano wa Ki-Bulgaria na daktari wa Kipalastina wakiwa kizimbani mahakamani nchini Libya
Wauguzi watano wa Ki-Bulgaria na daktari wa Kipalastina wakiwa kizimbani mahakamani nchini LibyaPicha: picture alliance/dpa

Kwa wauguzi hao watano na daktari mmoja lile janga walililokabiliana nalo sasa limemalizika. Lakini kwa Ulaya, kwa Ujerumani, mkasa huo haujamalizika, kwani lazima watu wajiulize namna gani katika siku za mbele wataingiliana na serekali kama ile ya Libya?

Ah! Mwisho umefikiwa. Machungu ya miaka minane walioyapata wauguzi watano wa Ki-Bulgaria na daktari wa Kipalastina sasa yamekwisha. Watu hao sita ambao huko Libya walishtakiwa kwa kuwaambukiza kwa makusudi watoto 400 virusi vya UKIMWI na mara mbili kuhukumiwa adhabu ya kifo na baadae kupewa kifungo cha maisha gerezani, sasa wameondoka Libya. Huo ni mwisho wa mkasa wenyewe. Na sasa ni hakika kwamba serekali ya Bulgaria haitawaweka vizuizini watu hao sita, kama vile mwanzoni ilivotakiwa na Libya.

Lakini kweli: jee huo ni mwisho wa mkasa wenyewe? Kuna haja mambo fulani kudurusiwa na kufafanuliwa kuhusu suala hili lisiloingia akilini. Na si lazima iwe mwanzoni kabisa, lakini inafaa kujuwa nani hasa aliechangia kwa sehemu kubwa kupatikana suluhisho hili, au wapi zimetokea fedha zilizopitishwa kulainisha ili kupatikane suluhisho? Inasemekana kumetolewa fedha nyingi, tena nyingi sana.

Huenda lililo muhimu kufafanuliwa hivi sasa ni lile suali: vipi dunia, na hasa Umoja wa Ulaya, katika siku za mbele zikabiliane na na serekali kama hizo. Mara nyingi utasikia kwa ukakamavu kutoka midomo ya wanasiasa wakitamka kwamba hawatakubali kubinywa pale yanapokuja masuala ya kutekwa nyara watu huko Afghanistan au Iraq, au kama karibuni yalipotolewa madai ya jumuiya za Kituruki hapa Ujerumani zikitaka iondoshwe ile sheria mpya ya uhamiaji. Na baada ya hapo unawacha Wajerumani katika mkasa kama ule wa Libya, wakikubali kubinywa. Tafauti, nayo ni tafauti kubwa, ni kwamba Libya ina mafuta, na ina gesi ya ardhini, na Ujerumani haina. Ili kujitoshekleza na mahitaji yao ya mafuta kwa msaada wa Libya, nchi za Magharibi, kama ni za Ulaya au Marekani, ziko tayari kusahau na kusamehe. Kusamehe na kusahau sio kitu kibaya, lakini kitu kibaya ikiwa kufanya hivyo kunafungamana na kulinda maslahi yako.

Kutokana na hali hiyo, hamu ya Libya ya kurejea katika jamii ya kimataifa imewezeshwa bila ya kuhakikisha kwamba serekali ya nchi hiyo kweli inabadilisha vitendo vyake. Kulipa fidia kwa wahanga wa ule mkasa wa kuangushwa ndege katika anga ya Lockerbie huko Scotland, kulipa fedha kwa ajili kuachiliwa huru mahabusu wa Kijerumani na kukomeshwa rasmi juhudi za Libya za kuwa na silaha za atomiki, yote hayo yameifanya nchi hiyo ya Afrika Kaskazini iweze kulainika tena.

Kwamba licha ya yote hayo, Libya bado ni nchi isiokuwa huru ni jambo ambalo hamna mtu alilolijali. Kwamba kunachorwa sura mbaya juu ya nchi hiyo kuhusu haki za binadamu na watu kukosa uhuru wa kutoa maoni yao- kwanini mambo hayo yaudhi inapokuja Libya, ambapo mambo kama hayo yanaonekana katika nchi nyingi? Lakini mambo ni kinyume na hivyo. Kwa kufanya hivyo mtu anakuwa anaisaidia serekali ya Libya kuuficha uchafu wake mbele ya wananchi wake. Ni wazi kwamba sio njama ya kidunia ya Wamarekani na Wazayuni iliokuwa nyuma ya kashfa hiyo ya virusi vya UKIMWI, lakini kashfa hiyo inatokana na hali mbaya ya kukosekana usafi katika hospitali walizokuwemo watoto hao.

Fedha ambazo zimechangia kulipwa familia za watoto hao walioambukizwa na virusi vya UKIMWI na kuusuluhisha mzozo huo, huenda, kwa hakika zaidi, zimetoka kwenye mfuko wa serekali ya Libya kuliko serekali za nchi za Ulaya. Matokeo gani yatakayochomoza kutokana na hali hii, ni jambo ambalo linafaa kufikiriwa kwa haraka, tena kwa kina. Kwa sasa, lakini, mtu anahitaji kufurahia kumalizika kwa mkasa huu. Umewadia wakati wa kufanya hivyo.