1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahaiti waizulia jambo UN

Admin.WagnerD19 Novemba 2010

Hali ya mambo inazidi kukorogeka nchini Haiti, ambapo watu wanawalaumu wanajeshi wa Umoja wa Mataifa kwa mripuko wa maradhi ya kipindupindu ambayo hadi sasa yameshasababisha zaidi ya vifo elfu moja.

https://p.dw.com/p/QDNj
Mwandamanaji akibeba bango linalosomeka "MINUSTAH na kipindupindu ni watoto pacha" wakati wa maandamano mjini Port-au-Prince, Haiti, Alkhamis ya Nov. 18, 2010. (Picha ya AP/Emilio Morenatti)
Mwandamanaji akibeba bango linalosomeka "MINUSTAH na kipindupindu ni watoto pacha" wakati wa maandamano mjini Port-au-Prince, Haiti, Alkhamis ya Nov. 18, 2010. (Picha ya AP/Emilio Morenatti)Picha: AP

Jasho. Machozi. Hasira. Mchanganyiko wa hamasa na hali ya kuvunjika moyo ndizo sentesi zinazosomeka kwenye nyuso za vijana wa Kihaiti. Hawamuamini yeyote, hawatarajii chochote. Hawana matumaini hata kwa chombo kikumbwa cha kimataifa, Umoja wa Mataifa, ambao kikosi chake cha MINUSTAH kimekuwapo hapa miaka nenda miaka rudi kulinda usalama. Sasa wanauona Umoja huu kuwa si chochote si lolote, zaidi ya sehemu ya matatizo yao. Wanaamini hata janga hili la kipindupindu limeletwa na wanajeshi wa Umoja huo.

Mmoja wa vijana hao Alexis, anasema kwa hasira kwamba kipindupindu kimeletwa na MINUSTAH, ambao wanataka kuwaua Wahaiti na kwamba lazima kikosi hicho kiondoke nchini mwao.

Mama wa Kihaiti akiwa amembeba mtoto wake mwenye dalili za ugonjwa wa kipindupindu
Mama wa Kihaiti akiwa amembeba mtoto wake mwenye dalili za ugonjwa wa kipindupinduPicha: AP

Jana (18 Novemba 2010) jioni hasira za vijana hawa zilianza kuvuuka mipaka ya kupiga kelele tu, na sasa kuwa uasi wa mitaani. Vizuizi vya barabarani, mawe, milio ya bunduki na mabomu ya machozi ndiyo matokeo yake. Mwanzoni mamia ya vijana walianza kwa kuwarushia mawe wanajeshi wa MINUSTAH waliokuwa kwenye gari, wanajeshi nao wakaelekeza bunduki zao kwa waandamanaji, na hapo ndipo hasira za vijana zikaongezeka maradufu.

Waandamanaji walikimbilia mitaani, lakini punde wakajikusanya tena, huku wengine wakiwa wamejifunika nyuso zao na sasa wakielekea moja kwa moja kwenye makao makuu ya MINUSTAH kilichoko Gourdon, lakini vikosi vya jeshi la Haiti vikaweka vizuizi njiani kuwazuia wasiende huko. Milio ya risasi ilisikika, ingawa haijulikani ilipotokea.

Kwengineko katika kambi ya Champ de Mars, ambako makumi kwa maelfu ya waathirika wa tetemeko la ardhi wamejihifadhi, vikosi vya jeshi vilitumia risasi za mipira kuwatawanya waandamanaji wengine, ambao nao wanaamini si Umoja wa Mataifa wala serikali yao ambayo imefanya ya kutosha kuzuia vifo vya watoto wao kutokana na kipindupindu.

Lakini afisa mmoja wa kimataifa anasema kwamba, ugonjwa huu wa kipindupindu unaweza ukawa umesababishwa na uchafu ulionea tangu nchi hiyo masikini ikumbwe na tetemeko la ardhi mwanzoni mwa mwaka huu, na "si lazima uwe umetokana na wanajeshi wa Umoja wa Mataifa" kama wanavyodai waandamanaji.

Lakini kuwafanya vijana hawa wa kimaskini ambao wameshavunjika moyo na maisha waamini kwamba ugonjwa huu unaoendelea kuchukua roho za dada na kaka zao hauna mkono wa mtu, ni suala litakalochukua muda.

Na hadi hapo haijuilikani ni hasara gani nyengine itakuwa imeshaikumba Haiti hii iliyokwishaumizwa na tetemeko, umasikini na machafuko.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFPE

Mhariri: Saumu Yusuf Ramadhan