1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahamiaji wa Kiafrika wateketea Mediterranean

Admin.WagnerD3 Oktoba 2013

Watu 94 wamefariki na wengine 250 hawajulikani walipo, baada ya boti iliyokuwa imejazwa na wahamiaji kutoka Afrika, kuzama karibu na kisiwa cha Lampedusa nchini Italia.

https://p.dw.com/p/19tNR
Baadhi ya miili ya wahamiaji waliofariki katika ajali ya boti kisiwani Lampedusa.
Baadhi ya miili ya wahamiaji waliofariki katika ajali ya boti kisiwani Lampedusa.Picha: picture-alliance/dpa

Kufuatia ajali hiyo, rais wa Italia Giorgio Napolitano ametoa rai ya kuimarisha ulinzi katika pwani za Afrika kaskazini ili kuzuwia wahamiaji kujaribu kuingia barani Ulaya. Napolitano ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa na Umoja wa Ulaya kushirikiana kukomesha usafirishaji haramu wa binaadamu, na kusisitiza kuwa haikubaliki kwamba Frontex, wakala wa Umoja wa Ulaya anaeshughulikia usalama wa mipakani haupewi vitendea kazi vya kutosha ili kuweza kuingilia kati pasipo kuchelewa.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia wakimbizi UNHCR, limesema karibu abiria 500, wengi wao wakiwa raia wa Eritrea walipanda boti hiyo nchini Libya, na askari wanaolinda pwani wamesema manusura 151 wameokolewa baada ya boti hiyo yenye urefu wa mita 20 kushika moto na kuzama yapatayo kilomita moja kutoka kisiwani Lampedusa.

Meya wa mji wa Lampedusa Giusi Nicolini ameielezea ajali hiyo kama maafa makubwa, na kuongeza kuwa miongoni mwa waliofariki alikuwepo mtoto mwenye umri wa miaka mitatu na mama mjamzito. Kisiwa cha Lampedusa kiko karibu zaidi na Afrika kuliko Italia bara, kikiwa umbali wa kilomita 113 kutoka pwani ya Tunsia, na ndiyo kimekuwa kituo cha mwisho kwa boti zinazosafirisha watu kwa njia za magendo. Meli za ulinzi wa pwani, boti za uvuvi na helikopta zilikuwa zinafanya msako katika bahari hiyo kutafuta manusura.

Wahamiaji wakiwasili katika kisiwa cha Lampedusa. picture alliance/ZUMAPRESS
Wahamiaji wakiwasili katika kisiwa cha Lampedusa.Picha: picture alliance/ZUMAPRESS

Chanzo cha ajali
Waziri wa mambo ya ndani wa Italia, Angelino Alfano aliwaambia waandishi wa habari kuwa boti hiyo ilianza kuzama baada ya kuzimika kwa injini yake moja, na abiria hawakuwa na simu kuweza kuomba msaada, na kwa hivyo waliwasha moto mdogo ili kuomba msaada kwa meli zilizokuwa zinapita.

Waziri Alfano ameongeza kuwa kwa kuwa gesi ilikuwa imechanganyika na maji yaliyoingia katika meli hiyo, moto ulisambaa katika meli yenyewe, na kuwalaazimu abiria kukimbilia upande mmoja, hatua iliyosababisha meli hiyo kupinduka na kuwamuaga abiria baharini. Hii ilikuwa ajali ya pili kutokea wiki hii karibu na Italia.

Siku ya Jumatatu wanaume 13 walizama wakati wakijaribu kuufikia mji wa Sicily,pale meli yao ilipopinduka ikiwa imebakiza mita chache kutia nanga. Papa Francis ambaye alitembelea kisiwa cha Lampedusa mwezi Julai katika ziara ya kwanza ya upapa nje ya jiji la Rome, alielezea kusikitishwa kwake na roho nyingi zilizoteketea katika ajali hiyo.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/ape, rtre, dpae.
Mhariri: Josephat Nyiro Charo