1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahanga wa 'Holocaust' wakumbukwa

Mohammed Abdulrahman
27 Januari 2017

Tarehe 27 Januari ni siku ya kuwakumbuka wahanga wa mauaji makubwa ya kimbari dhidi ya wayahudi yaliofanywa na utawala wa Adolf Hitler, kutokana na sera yake aliyoiita ya uzalendo wa Kisoshalisti.

https://p.dw.com/p/2WUlF
Deutschland Holocaust Gedenkstunde des deutschen Bundestages Malu Dreyer, Jaochim Gauck, Angela Merkel, Andreas Vosskuhle
Kansela Angela Merkel (wa pili kulia) na rais wa shirikisho Joachim Gauck (wa pili kushoto) wakishiriki kumbukumbu hiyo katika bunge la Ujerumani Bundestag Januari 27.01.2017.Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Sohn

Mtawala huyo alipalilia  fikra ya kuondokana na  kile alichokiita udhaifu na uwoga miongoni mwa Wajerumani. Matokeo yake akasababisha kupotea kwa maisha ya ummati mkubwa wa watu ndani ya Ujerumani na  katika nchi zilizokaliwa na wanazi. Lakini mauaji hayo yasingefikia idadi  kubwa kama si kuhusika kwa madaktari, majaji, maafisa wa shughuli za utawala, wanasayansi na wengine.Palitumika kile kilichoitwa utafiti wa  nasaba ambapo ilihusishwa sayansi na  siasa. Maike Rotzoll , Naibu Mkurugenzi wa taasisi ya Historia na  Maadili ya masuala ya Tiba ilioko katika mji wa Halle, ameiambia Deutsche Welle kwamba, maafisa wa utawala wa  wanazi walijaribu kuzigeuza fikra zao kuwa  ukweli wa kisiasa na kwa hakika walifanikiwa.

Hitler na wafuasi wake walianza kushinikiza  ajenda yao mara tu baada ya kuingia madarakani Januari 30,  1933. Ilipofika mwezi Julai mwaka huo, Baraza la mawaziri la Hitler likapitisha sheria kuhusu vinasaba vya urathi. Sheria hiyo ikalifanya jambo la lazima kutolewa kizazi mtu yeyote aliyekuwa na uwezekano wa kupata watoto ambao watakua na  athari kama  za kiakili, mfadhaiko, uziwi, na  hali nyengine za ulemavu . Mahakama za Ujerumani wakati huo zikawa zikitekeleza  ushauri  na mapendekezo ya madaktari na maafisa wa afya kwa jumla juu ya kuwaondolea uwezo wa kuzaa. Mahakama maalum za suala hilo, zikaidhinisha 90 asilimia ya matakwa ya aina hiyo na  watu laki tatu hadi nne, wengo kutoka taasisi za magonjwa ya akili  wakaondolewa uwezo wa kuzaa kabla ya vita vya  vikuu vya pili vya Dunia. Wengine wakauawa baadae.

Deutschland Touristen am Holocaust-Mahnmal in Berlin
Watalii wakipiga picha kwenye kituo cha kumbukumbu ya mauaji ya Wayahudi mjini Beerlin, Ujerumani.Picha: DW/N. Wojcik

Kutoka kwenye kuondolewa  uzazi hadi kuuwawa:

Mwezi Oktoba 1939, madaktari na wauguzi wakapewa amri kuwahamishia watoto wote wenye  ulemavu na kasoro nyengine kiafya kwenye  hospitali maalum ambazo ziligeuzwa  kuwa  maeneo ya kifo. Mpango huo uliongozwa na  Philipp Bouhler, mkurugenzi wa ofisi  ya binafsi ya hitler pamoja na Karl brandt mmoja wa madkatari binafsi wa Hitler. Mpango huo ukijulikana kama T-4 kifupisho cha mtaa ulioitwa Tiergartenstrasse nambari 4 mjini Berlin, mahala pa ofisi iliowaajiri na kuwalipa walioshiriki katika mauaji hayo.

Ilipofika  1940, kulikuwa tayari kuna vituo 6 vilivyoundwa katika sehemu tafauti za Ujerumani. watu 70,273 waliuwawa, wahanga walipewa sumu, waliwekwa na njaa hadi kufa pamoja na  mpango huo wa T-4  kutumia vyumba vya mauaji kwa klutumia gesi, mpango uliotangulia mauaji  katika kambi ya Auschwitz ba kambi nyengine za mauaji . Kwa mtazamo huo, mauaji hayo huchukuliwa kuwa maandalizi ya kile kilichowasibu  wayahudi baadae yaani mauaji ya kimbari (Holocaust) .

Lawama na upinzani:

Watu  zaidi ya  100,000 waliuwawa kama sehemu ya  mpango wa T-4 ambao ulisitishwa Agosti 1941.Mauaji hayo yakasababisha malalamiko na upinzani hasa kutoka kwa Wakatoliki waliohisi yalikuwa kinyume na  mafundisho ya dini yao. Kwa muda mrefu wan ahistoria waliandika kwamba hitler alilazimika kuufuta mpango huo kutokana na shinikizo la  umma. lakini uvamizi wa Ujerumani nchini Urusi Juni 1941 ulimaanisha kuwa wengi miongoni mwa watekelezaji wa T-4 wakihitajika katika  maeneo yaliokaliwa ya Ulaya Mashariki kwa ajili ya mpango  mkubwa zaidi wa mauaji, na hasa katika maeneo yaliotekwa na Ujerumani ya Wanazi  wakati wa vita. Wanahistoria wanataja idadi ya wahanga kuwa karibu 300,000. wauaji wakatumika  kufanya kazi hiyo katika kambi za wafungwa za Sobibor na Treblinka. 

Kumaliza Ukimya:

Kwa muda mrefu katika Ujerumani ya baada ya vita, waliuwawa kutokana na mpango wa mauaji walikuwa wahanga wa Wanazi waliosahauliwa. Familia zikisita kuwakumbuka jamaa zao  waliokufa, huwenda ni kwa sababu ya aibu ya kushindwa kuwalinda, au kwa sababu ya ulemavu  waliokuwa nayo baadhi yao wakiwemo wagonjwa wa akili. Lakini miaka  baadae, Wajerumani- wanahistoria na wana dini- walianza kuibua kadhia  za wahanga wa mauaji  na maovu hayo.

Deutschland Holocaust Gedenken zum 72. Jahrestag der Befreiung von Auschwitz
Manusura wa mauaji ya mauaji ya wayahudi akifuta machozi wakati wa kumbukumbu ya miaka 72 ya mauaji hayo.Picha: picture-alliance/dpa/A. Grygiel

Mwandishi Sigrid Falkstein  kwa mfano,  ambaye alizaliwa 1946, alishtushwa alipokuja kufahamu kwamba shangazi yake Anna Lehnkering aliuwawa katika  kambi ya  Grafeneck na hilo lilimpa ujasiri Falkstein kuandika kitabu kilichoitwa" Kumfuatilia Anna."

Aliiambia Deutsche Welle," Katika familia yangu hatukuwa tukizungumza kabisa kuhusu Shangazi yangu." Hivi sasa ninajua familia yangu ilikubwa na  mchanganyiko wa mfadhaiko, ukimba na suala hilo kuwa  mwiko." Kwa muda mrefu wahanga  wote na walionusurika na familia zao-  Magharibi na Mashariki mwa Ujerumani, walipigwa na hofu na   mshtuko na kulazimika kunyamaza na kutodhukuru yaliotokea. Kwa upande mwengine  kwa bahati mbaya, wengi wa wahusika katika ovu huo waliepuka kuadhibiwa na hivyo wakawa huru na kuendelea na shughuli zao.

Kuwapa heshima  wahanga:

Falkenstein ambaye atazungumza katika bunge la Ujerumani katika hafla ya kuwakumbuka wahanga wa mpango wa mauaji mauaji wa Hitler wa walioonekana kutokuwa na faida  katika jamii kutokana na ulemavu  anasema, amepokea  maelezo mengi ya kumpongeza kutoka kwa familia za wahanga ambazo zilipata moyo wa kutafuta ukweli kuhusu jamaa zao, baada ya kukisoma kitabu chake. Anasema,"Pengine nimeweza kutchangia kwa namna fulani kulifanya suala hili kufahamika kwa upana zaidi. Ni tukio  la kishitoria, tukio la kukandamizwa haki, pengine  tu kwa sababu wahanga walikuwa ni watu waliotazamwa kwa jicho jengine.  Falkstein anasema kisa cha shangazi yake kinaonyesha kile kinachoweza kutokea pale tunapowaangalia watu  kwa  thamani  na umuhimu wao na kuwatenga wengine kwa sababu tu ya mapungufu walio nayo -ulemavu katika miili yao. Hayo yalitangulia mauaji ya kimbari -mwanzo wa  kile kinachojulikana kama Holocaust, ambapo jumla ya wayahudi milioni 6 waliuwawa.

Mwaka 2014, makumbusho maalum  kuhusu wahanga wa T-4 ilifunguliwa katika mtaa wa Tiergarten nambari 4. Hafla  ya kumbukumbu  katika bunge la Ujerumani Bundestag, ni hatua moja mbele ya kuwapa  heshima wahanga wa mpango wa mauaji wa Hitler na nafasi yao  wanayostahiki katika historia.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, Chase Jafferson

Mhariri:Yusuf Saumu

LINK: http://www.dw.com/a-37286088