1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri wanazungumzia juu ya mauaji ya madaktari Afghanistan.

Abdu Said Mtullya9 Agosti 2010

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanaonya dhidi ya kuyaondoa majeshi baada ya kuuawa madaktari wa kimataifa nchini Afghanistan.

https://p.dw.com/p/OfZb
Ndugu wa mfanyakazi wa shirika la misaada wakibeba maiti ya ndugu yao alieuawa na Taliban nchini Afghanistan.Picha: AP

Madaktari na wahudumu wa afya wa shirika la misaada la International Assistance Mission waliuawa kaskazini mwa Afghanistan na waliowaua wanadai kwamba watu hao walikuwa wanaeneza ukristo nchini Afghanistan.

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanatoa maoni yao juu ya mkasa huo.

Mhariri wa gazeti la Mannheimer Morgen anapinga vikali madai hayo yaliyotolewa na Taliban wanaosema kuwa wao ndio waliowaangamiza madaktari na wahudumu hao wa afya.Katika maoni yake, mhariri wa gazeti hilo anasema labda mtu anaweza kujiuliza iwapo shirika la misaada la madaktari hao lilivuka mipaka fulani, na hivyo kuyahatarisha maisha ya wafanyakazi wake.Lakini kudai kwamba madaktari hao walikuwa na biblia mikononi wakieneza ukristo kwa njia ya kificho, siyo jambo la kweli asilani.

Mhariri huyo anasisitiza kwamba awali ya yote,kazi inayofanywa na shirika la misaada la madaktari hao ni kutoa huduma za afya.Kwa hiyo, shirika hilo linapaswa kuendelea na shughuli za kuwasaidia watu wa Afghanistan.

Lakini gazeti la Braunschweiger linasema shirika la misaada la wahudumu hao wa afya linapaswa kuwa na uangalifu katika utekelezaji wa kazi zake nchini Afghanistan.Mhariri wa gazeti hilo anasema,baada ya kuuawa madaktari wake, shirika hilo sasa litapaswa kubadili njia inazozitumia katika kutekeleza kazi zake.Hadi sasa shirika hilo limekuwa linakataa wafanyakazi wake walindwe na askari, kwa kutumai kwamba wana imani ya watu wa Afghanistan.Gazeti linasema hilo ni kosa!

Mhariri wa gazeti la Brauschweiger anasema shirika hilo la misaada linahitaji ushauri juu ya usalama wa wafanyakazi wake na ikiwezekana wahudumu hao wapewe ulinzi na watu wenye silaha.

Gazeti la Fränkischer Tag linawaambia watu wa Afghanistan kwamba lengo la Wataliban ni kupora mamlaka, na wapo tayari hata kuzuia kutolewa huduma muhimu kwa wananchi.

Gazeti hilo linafafanua kwa kusema wahalifu wa Kitaliban wanaitumia vibaya dini ya kiislamu ili kufanikisha lengo lao, yaani kurejesha utawala wa kidikteta nchini Afghanistan.Na ndiyo sababu hawataki kuona hata misaada kutoka nje ,japo misaada hiyo ni muhimu kwa wananchi.

Watu wa Afghanistan sasa wanaweza kuona dhahiri kwamba wahudumu wa afya waliouliwa na Taliban siyo maadui wa watu wa Afghanistan.

Gazeti la Flensburger linawatahadharisha wanasiasa wanaotoa miito juu ya kuyaondoa majeshi kutoka Afghanistan kwa kueleza kuwa

hatua kwa hatua, Wataliban wanaueneza mtandao wao wa mabavu muda mrefu baada ya kutimuliwa mnamo mwaka wa 2001. Kwa hivyo, anaezungumzia juu ya kuyaondoa majeshi kutoka Afghanistan ajue kuwa siyo tu kwamba anawatosa watu wa Afghanistan, bali pia anayafuta yote yaliyokwishatimizwa hadi sasa nchini Afghanistan.

Mwandishi/Mtullya Abdu /Duetsche Zeitungen.

Mhariri: Miraji Othman