1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri watoa maoni juu ya mgogoro wa Ugiriki

Abdu Said Mtullya9 Juni 2011

Ujerumani inataka sekta binafsi pia ishiriki katika awamu ya pili ya kuisaidia Ugiriki

https://p.dw.com/p/11XWz
Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang SchäublePicha: dapd

Katika maoni yao wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanauzungumzia mgogoro mkubwa wa madeni unaoikabili Ugiriki na hatua zinazochukuliwa na Ujerumani ili kuisadiai nchi hiyo. Ugiriki inahitaji kupigwa jeki kwa mara ya pili la sivyo nchi hiyo itafilisika. Ujerumani ndiyo itakayotoa sehemu kubwa ya msaada huo lakini sekta binafsi pia ihusishwe.

Ujerumani ina wasiwasi, kama anavyosema mhariri wa gazeti la Neue Osnabrücker. Anatilia maanani kauli zinazotolewa na baadhi ya wataalamu wa Ujerumani juu ya kuifungia Ugiriki njia zote za fedha. Lakini mhariri huyo anasema serikali ya Ujerumani ina wasiwasi na inadhamiria kuepusha maafaa.

Mhariri wa gazeti la Märkische pia anasisitiza juu ya msimamo wa serikali ya Ujerumani katika juhudi za kuisaidia Ugiriki kukabiliana na mgogoro wake mkubwa wa madeni. Mhariri huyo anaeleza kuwa Waziri wa fedha wa Ujerumani amependekeza hatua ya kuubadili utaratibu unaotumiwa na Ugiriki katika kuyalipa madeni yake. Waziri huyo bwana Wolfgang Schäuble anataka sekta binafsi pia ishiriki katika awamu ya pili ya kuisaidia Ugiriki.

Gazeti la Stuttgarter Nachrichten pia linalitilia maanani pendekezo la waziri wa fedha wa Ujerumani juu ya kuinusuru Ugiriki. Gazeti hilo linasema pendekezo la Waziri Schäuble ni sahihi kwa sababu hatimaye mzigo, utabebwa na pande zote, badala ya walipa kodi tu. Waziri huyo amesema ndiyo, utakuwapo mpango wa pili wa kuisaidia Ugiriki, lakini nguvu ya watu binafsi pia inahitajika.

Gazeti la Lübecker Nachrichten linatumia maneno makali juu ya Ugiriki kwa kusema kwamba nchi hiyo haikustahili kuwamo katika Umoja wa sarafu ya Euro, lakini linasisitiza kwamba nchi hiyo inahitaji kusaidiwa. Linasema pamoja na kosoro zote, Ugiriki ni mwanachama wa jumuiya ya nchi zinazotumia sarafu ya Euro. Kwa hiyo nchi hiyo inahitaji kusaidiwa la sivyo itageuka kuwa kitongoji cha walalahoi barani Ulaya na itageuka kuwa bakteria wa E Coli mnamo sarafu ya Euro!

Gazeti la Lübecker Nachrichten linakumbusha historia ya benki ya Lehman ya nchini Marekani. Linasema yafaa kujifunza kutokana na makosa ya Marekani. Wakati benki ya Lehman ilipofilisika, serikali ya Marekani ilidiriki kufanya majaribio kwa kuicha benki hiyo iyatatue matatizo yake yenyewe. Lakini majaribio hayo yalisababisha vurumai katika mfumo wote wa fedha duniani. Mfumo wa fedha wa dunia ulikaribia kusambaratika kwa ndani.

Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/.

Mhariri/-