1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waislamu duniani waadhimisha siku kuu ya Eid ul Fitr

Iddi Ssessanga
15 Juni 2018

Waislamu kote duniani wamesherehekea siku kuu ya Eid ul Fitr, ambayo ndiyo ishara ya kumalizika kwa funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Kufunga mwezi wa Ramadhan ni mmoja ya nguzo kuutano za dini ya Kiislamu.

https://p.dw.com/p/2zcPS
Zuckerfest Bonn Bonsiaken
Picha: DW/M. Smajic

Zaidi ya Wapalestina elfu 90 wamehudhuria ibada hiyo wekyen msikiti wa Al-Aqsa mjini Jerusalem, ambapo mufti wa mji huo ameukosoa mpango wa amani wa rais wa Marekani Donald Trump katika hotuba yake. Sheikh Muhammad Hussein amesema mpango huo ni usiyo wa haki wenye lengo la kuzima ndoto za Wapalestina.

Trump ameahidi kile alichokiita makubaliano ya mwisho kati ya israel na Wapalestina, na anatarajiwa kutangaza mpango huo katika siku za usoni. Hatua ya Trump kuuhamisha ubalozi wa Marekani nchini Israel kutoka Tel Aviv kwenda Jerusalem iliwakasirisha Wapalestina wanaoiona hatua hiyo kama kuegemea upande wa Israel katika suala nyeti la mgogoro wa mashariki ya Kati.

Wanasema hatua hiyo iliiondolea Marekani sifa ya kuwa mpatanishi wa mgogoro huo. Mjini Ghaza, kiongozi wa kundi la Hamas Ismail Haniya aliungana na waumini waliofanya ibada ya swala mashariki mwa ukanda huo karibu na mpaka wa Israel, ambapo alizungumzia kura iliopigwa katika baraza kuu la Umoja wa Mataifa kulaani mauaji ya Israel dhidi ya Wapalestina wakati wa maandamano ya hivi karibuni.

Zuckerfest Bonn Bonsiaken
Waislamu wakisikiliza htuba katika msikiti mmoja mjini Bonn, Ujerumani.Picha: DW/M. Smajic

"Kilichotokea katika Baraza kuu la Umoja wa Mataifa kinaonyesha kuwa maandamano ya kudai haki ya kurejea na kuvunja mzingiro yamehuisha suala la Palestina na  kuliweka suala hilo kwenye ajenda ya kimataifa. Napenda kuzishukuru nchi zote za Kiarabu na Kiislamu na dunia kwa ujumla ziliunga mkono haki ya Wapalestina na kusimama nasi," alisema Haniyeh.

Assad aswali nje ya Damascus

Nchini Syria, rais Bashar al-Assadmamehudhuria swala ya Eid katika msikiti mjini Tartous, ulioko katika mkoa wa pwani ambao umemuunga mkono rais huyo katika kipindi chote cha vita vya wenyewe kwa wenyewe vlilivyodumu kwa miaka saba sasa.

Na nchini Iran, kiongozi wa juu wa taifa hilo Ayatollah Ali Khamenei, aktika hotuba yake ya sherehe za Eid amewasifu raia kwa kuhudhuria kwa wingi mikutano ya hadhara Ijumaa iliopita kuwaunga mkono Wapalestina wakati wa Qudsi, au siku ya Jerusalem. Siku hiyo ilianzishwa na Iran mwaka 1979 kuonyesha mshikamano na Wapalestina na kuipinga Israel.

Kutoka Mjini Kabul, rais wa Afghanistan Mohammad Ashraf Ghani ameusifu mpango wa siku tatu wa kusitisha mapigano na kundi la Taliban katika hotuba yake kwa taifa. Ametumia fursa hiyo kuomba kuwepo na usitishaji wa muda mrefu na kutoa wito kwa Taliban kushiriki mazungumzo badala ya kurudi katika uwanja wa vita.

Zuckerfest Bonn Bonsiaken
Qur'aan ambayo ndiyo muongozo wa maisha ya Muislamu.Picha: DW/M. Smajic

Misri wakabiliwa na ugumu wa maisha

Wamisri wamesherehekea siku hii mnamo wakati serikali ya rais Abdel-Fatah el-Sissi ikiendelea na hatua kali za kubana matumizi ambazo zimesababisha kupanda kwa bei za bidhaa. Hatua hizo ambazo zinahusisha kupunguzwa kwa ruzuku za mafuta na umeme, kuweka kodi ya ongezeko la thamani ni sehemu ya programu ya mageuzi inayohusiana na mkopo wauokozi wa dola bilioni 12 kutoka shirika la fedha la kimataifa IMF.

Katika mataifa mengi ya Kiislamu, miji mikuu ilipambwa na taa za usiku kuashiria kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani, ambao ni moja ya nguzo kuu tano za dini ya Kiislamu. Nguzo hizo tano ndiyo majukumu matano makuu ambayo Muislamu yeyote anapaswa kuyatimiza ili kushi maisha yanayofuata Uislamu.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape,afpe,

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman