1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waisrael na Wapalastina watakiwa wajizuwie

Oumilkheir Hamidou
5 Aprili 2018

Hali inatisha katika mpaka wa Ukanda wa Gaza, katika wakati ambapo Wapalestina wanajiandaa kwa wimbi jengine la maandamano. Mjumbe wa Umoja wa Mataifa amezisihi pande zote mbili, Waisrael na Wapalestina wajizuwie.

https://p.dw.com/p/2vYOF
Palästina Proteste Gaza Streifen
Picha: Reuters/M. Salem

 

Katika pande zote mbili za mpaka wa Gaza, watu wanajiandaa kwa wimbi jengine la maandamano makubwa ya Wapalestina yaliyopangwa kuitishwa siku ya Ijumaa, wiki moja baada ya mapambano pamoja na wanajeshi wa Israel kusababisha damu nyingi  kabisa kumwagika, tukio ambalo halijawahi kushuhudiwa tangu miaka kadhaa iliyopita. Idadi jumla ya waliouwawa inafikia watu 21  baada ya bwana mmoja kufariki dunia kutokana na majeraha-wizara ya afya ya Gaza imesema. Idadi ya wahanga ilifikia watu 20 baada ya kijana wa miaka 34 kuuliwa kwa mizinga ya ndege za kivita za Israel, alipokuwa anakurubia  uzio wa usalama uliowekwa na Israel huko Gaza.

"Vikosi vya usalama vya Israel havitomruhusu yeyote kudhuru usalama wa raia wa Israel na vitaendelea kupambana na magaidi wanaohusika na visa vya kigaidi" jeshi la Israel limesema katika taarifa yake.

Ofisi kuu ya uwiano pamoja na Wapalestina , imewaonya Wapalastina dhidi ya madhara ya kimazingira yanayotokana na kutiwa moto mipira ya magari, huku waziri wa usalama wa jamii Gilad Erdan akisema  maandamano yatakuwa na madhara kwa wakaazi wote wa Gaza.

Wanajeshi wa Israel waakizuwia maandamano huko Hebrone
Wanajeshi wa Israel waakizuwia maandamano huko HebronePicha: picture alliance/AA/M. Wazwaz

 B'Tselem lawataka wanajeshi wa Israel wasitii amri ya kufyetua risasi

Shirikia linalopigania haki za binaadam nchini Israel B'Tselem limewatolea wito wanajeshi wasiwafyetulie risasi waandamanaji kesho ijumaa na ikilazimika, wapuuze amri ya viongozi wao."Ni kinyume na sheria kuwafyetulia risasi waandamanaji wasiokuwa na silaha na amri kama hiyo ni kinyume na sheria, shirika hilo limesema katika taarifa yake.

Maelfu ya Wapalestina waliongozana wakibeba bendera na kupiga kambi karibu na mpaka wiki iliyopita kwa kile walichokiita "Maandamano makubwa ya kurejea nyumbani"-maandamano yatakayodumu wiki sita hadi Mei 15, siku ambayo Israel itaadhimisha miaka 70 tangu ilipoundwa huku Wapalestina nao wakikumbuka siku waliyotolewa katika maskani yao au Al Nakba, neno la kiarabu linalomaanisha "Balaa."

Wakaazi wa Gaza wakipaza sauti kudai haki ya wapalastina kurejea nyumbani
Wakaazi wa Gaza wakipaza sauti kudai haki ya wapalastina kurejea nyumbaniPicha: Reuters/I. A. Mustafa

Maandamano makubwa zaidi yahofiwa kutokea kesho katika maeneo ya utawala wa ndani wa Palastina

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa katika eneo la mashariki ya kati Nickolay Mladenov ameihimiza Israel "ijizuwie na kuwataka Wapalestina waepukane na ugonvi wakati wa maandamano yao katika eneo la mpakani la Gaza. Wito wa Nickolay Mladinov umetolewa katika wakati ambapo hofu zimeenea za kuzuka machafuko makubwa zaidi baada ya sala ya ijumaa. Mladenov amewataka pia wanajeshi wa Israel wajizuwie huku Wapalestina akiwasihi waepukane na ugonvi katika eneo la mpakani. Maandamano na malalamiko lazima yaruhusiwe kuendelea kwa njia ya amani. Raia na hasa watoto wasitiwe hatarini kwa njia yoyote ile, amesisitiza.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa/Reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga