1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waisraeli na Wapalestina warejee katika majadiliano

20 Machi 2010

<p>Majadiliano ya amani kati ya Israel na Wapalestina yaliyokwama, huenda yakaanza upya hivi karibuni. Hiyo ni kwa mujibu wa wapatanishi wa kimataifa waliokutana Moscow nchini Urusi siku ya Ijumaa.<p>

https://p.dw.com/p/MY2L
U.S. Secretary of State Hillary Rodham Clinton waves upon arrival in Moscow's Vnukovo airport on Thursday, March 18, 2010. Hillary Rodham Clinton is in Moscow to meet with senior Russian officials and to join top international diplomats in assessing the stalled Mideast peace process.(AP Photo/Ivan Sekretarev)
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton akiwasili Moscow kwa majadiliano ya kuhimiza mchakato wa amani wa Mashariki ya kati uliokwama.Picha: AP

Wajumbe wa Marekani,Umoja wa Mataifa,Umoja wa Ulaya na Urusi - maarufu kama kundi la pande nne- walikutana kujadili mapendekezo mapya, kwa azma ya kuwarejesha Wapalestina na Waisraeli katika meza ya majadiliano.

Mjumbe maalum katika Mashariki ya Kati, Tony Blair amesema, ni matumaini yake kuwa karibuni utapatikana mpango utakaoanzisha majadiliano yasio ya uso kwa uso. Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amewahimiza Waisraeli na Wapalestina kutekeleza wajibu wao katika jitahada za kutafuta amani.

U.N. Secretary General Ban Ki-moon, left, and Russian President Dmitry Medvedev enter a hall for talks in Moscow's Kremlin on Thursday, March 18, 2010. (AP Photo/RIA Novosti, Mikhail Klimentyev, Presidential Press Service)Ban
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon(kushoto) na Rais wa Urusi,Dmitry Medvedev.Picha: AP

Lakini, pendekezo lililotolewa kwa Israel na Wapalestina kuanzisha majadiliano ya amani na kupata suluhisho la mataifa mawili, limepokewa kwa maoni mbali mbali. Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Avigdor Liebermann alipozungumza ziarani mjini Brussels alisema, Israel haitokubali kushinikizwa kwa kile alichokiita "kanuni za bandia na kipindi kisichozingatia hali halisi." Wakati huo huo, mpatanishi mkuu wa Wapalestina, Saed Erakat ameuliza vipi itahakikishwa kuwa Israel kweli itasitisha ujenzi wa makaazi ya walowezi. 

Wajumbe wa kundi hilo la pande nne wameitaka Israel isitishe moja kwa moja ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi katika maeneo inayoikalia na kurejea katika meza ya majadiliano. Lengo ni kupata mkataba kuhusu taifa la Palestina lililo huru na lenye uwezo wa kuendelea kuwepo. Wamesema, mkataba huo upatikane katika kipindi cha miezi 24 ijayo.

Mwandishi:Martin,Prema/ZPR

Mhariri: Mwadzaya,Thelma