1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Wajumbe wa Hamas waondoka mjini Cairo

Tatu Karema
7 Machi 2024

Kundi la wanamgambo la Hamas limesema kuwa wawakilishi wake wanaoshiriki mazungumzo ya kusaka usitishaji mapigano katika Ukanda wa Gaza wameondoka mjini Cairo nchini Misri na kwamba mazungumzo hayo yataendelea wiki ijayo

https://p.dw.com/p/4dGim
Mkuu wa kundi la Hamas katika ukanda wa Gaza  Yehya al-Sinwar wakati wa maandamano ya kuadhimisha miaka 35 tangu kuundwa kwa kundi hilo mnamo Desemba 14, 2022
Mkuu wa kundi la Hamas katika ukanda wa Gaza - Yehya al-SinwarPicha: Mohammed Abed/AFP

Afisa mmoja mkuu wa Hamas amethibitisha leo kwamba wawakilishi wa kundi hilo katika mazungumzo hayo ya amani ya Gaza wameondoka Cairo kuelekea mjini Doha nchini Qatar kwa mashauriano, huku akielezea kutoridhishwa kwake na majibu ya Israel kufikia sasa.

Afisa huyo ambaye hakutaka kutambulishwa amesema kuwa wanasubiri jibu rasmi kutoka Israel.

Hamas yasema Israel haijatoa hakikisho kuhusu usitishaji mapigano

Msemaji wa kundi laHamas, Jihad Taha, amesema Israel imekataa kujitolea na kutoa hakikisho kuhusu usitishaji wa mapigano katika Ukanda wa Gaza, kurejea kwa Wapalestina waliolazimika kuyakimbia makaazi yao na kuondoa vikosi vyake kwenye Ukanda huo.

Soma pia:Hamas yasema itaendelea na mazungumzo ya usitishaji vita

Hata hivyo Taha, amesema mazungumzo hayo bado yanaendelea na vikao vyake vitaanza tena wiki ijayo.

Hakukuwa na jibu la haraka kutoka Israel.

Mazungumzo yakwama kutokana na masharti ya Hamas

Awali, maafisa wa Misri walikuwa wamesema kuwa mazungumzo hayo yalikwama kutokana na masharti ya Hamas ya mchakato wa hatua kwa hatua ambayo baadaye yaliishia kwa sharti la kusitishwa kwa vita.

Soma pia:Israel yauwa Wapalestina zaidi ya 100, yajeruhi zaidi ya 700

Lakini maafisa hao hawakufutilia mbali uwezekano wa kufikia makubaliano kabla ya kuanza kwa mwezi huo mtukufu wa Ramadhani siku ya Jumapili, ambao unachukuliwa kama tarehe ya mwisho isiyo rasmi ya kufikia makubaliano hayo.

Shambulizi la jeshi la Israel lasababisha vifo vya wapiganaji 17 Gaza

Jeshi la Israel limedai kuwa shambulizi lake la anga limesababisha vifo vya wapiganaji 17 katika maeneo ya Kusini na Kati mwa Gaza. 

Majengo yalioporomoka kutokana na shambulizi la anga la Israel mjini Khan Yunis mnamo Machi 6 2024
Majengo yalioporomoka kutokana na shambulizi la anga la Israel mjini Khan YunisPicha: Bashar Taleb/APA images/IMAGO

Vikosi vya ardhini vya Israel vinasema vimeshambulia kamandi za kundi la Hamas na malango ya mahandaki, ambapo vinadai kugundua maeneo ya kutengeneza silaha na maghala ya vifaa vya kijeshi vya kundi hilo ambalo Israel, Marekani na Umoja wa Ulaya zimeliorodhesha miongoni mwa makundi ya kigaidi.

Soma pia:Vita vya Gaza vyatishia mzozo mkubwa Mashariki ya Kati

Zaidi ya miezi minne baada ya kuanza kwa mashambulizi ya ardhini katika Ukanda wa Gaza, vikosi vya Israel havijaweza kumkamata mkuu wa Hamas katika eneo hilo, Yehya al-Sinwar.

Pia hakuna dalili ya mateka takriban 100 wa Israel waliotekwa na kundi la Hamas na makundi mengine wakati wa uvamizi wa kushtukiza wa Oktoba 7 kusini mwa Israel.

Israel yaishtumu Afrika Kusini kwa kujifanya kama kitengo cha kisheria cha Hamas

Wakati huo huo, Israel, imeishtumu Afrika Kusini kwa kujifanya kama kitengo cha kisheria cha Hamas baada ya nchi hiyo kwa mara nyingine tena kuwasilisha ombi kwenye Mahakakama ya Kimataifa ya Haki, ICJ, kuitaka kuchukuwa hatua dhidi ya Israel.

Soma pia:Afrika Kusini yaitaka ICJ kuishinikiza Israel kuhusu Gaza

Wizara ya mambo ya nje ya Israel imesema kuwa Afrika Kusini inaendelea na juhudi za kuhujumu haki yake ya kimsingi ya kujilinda pamoja na raia wake na kuachiwa huru kwa mateka wake wote.

Hata hivyo msemaji wa serikali ya Afrika Kusini amepuuzilia mbali madai hayo.