1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wajumbe wa Saudi Arabia na Oman kuzungumza na Wahouthi

Zainab Aziz
9 Aprili 2023

Wajumbe wa Saudi Arabia na Oman wamewasili kwenye mji mkuu wa Yemen, Sanaa kwa ajili ya mazungumzo na kiongozi wa baraza kuu la kisiasa la Wahouthi.

https://p.dw.com/p/4PrAv
Jemen Sanaa Anschläge
Picha: Mohammed Hamoud/AA/picture alliance

Wajumbe wa Saudi Arabia na Oman wamewasili kwenye mji mkuu wa Yemen, Sanaa kwa ajili ya mazungumzo na kiongozi wa baraza kuu la kisiasa la Wahouthi. Shirika la habari la Wahouthi, Saba, limenukuu chanzo kilichosema kuwa wajumbe hao watajadili njia za kuondoa mzingiro, kukomesha vita na kurejesha haki za watu wa Yemen ikiwa pamoja na kulipa mishahara ya wafanyakazi wote wa serikali kutokana na mapato ya mafuta na gesi. Hapo jana, Saudi Arabia iliwaachia mateka wa vita 16 wa Kihouthi. Mateka hao waliachiwa wakati wajumbe wa Oman walipowasili nchini Yemen ikiwa ni sehemu ya juhudi za jumuiya ya kimataifa za kuvimaliza vita vya nchini Yemen ambavyo vimeshachukua muda mrefu. Shirika la habari la AP limeripoti kwamba makubaliano ya kuachiwa mateka wa vita yaliyofikiwa kwa upatanishi wa Umoja wa Mataifa mwezi uliopita yatajumisha wapiganaji wapatao 900 wa pande zote zinazohusika na mgogoro wa nchini Yemen. Makubaliano hayo yanatarajiwa kutekelezwa mnamo mwezi huu.