1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanadiplomasia wabishana vikali kwenye Baraza la Usalama

Zainab Aziz
4 Januari 2019

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa aliyeamriwa kuondoka nchini Somalia asema taifa hilo linakabiliwa na machafuko ya kisiasa huku balozi wa Somalia akilitaka Baraza la Usalama kuacha kuingilia mambo ya ndani ya nchi yake.

https://p.dw.com/p/3B2wu
UN Sicherheitsrat Yemen
Picha: Reuters/C. Allegri

Wakizungumza kwenye kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Alhamis  Januari 3, wanadiplomasia hao walitoa kauli zinazohitafiliana, siku mbili baada ya Somalia kumuamuru Nicholas Haysom kuondoka nchini humo, ikimtuhumu kwa kukiuka mipaka ya kazi yake.

Haysom aliliambia Baraza la Usalama kwamba hali ya kisiasa nchini Somalia inatishia kulitumbukiza tena taifa hilo kwenye machafuko makubwa. Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa alifukuzwa baada ya kuhoji kukamatwa kwa watu kadhaa, akiwemo Mukhtar Robow, kiongozi wa zamani wa kundi la kigaidi la al-Shabaab. Balozi wa Somalia kwenye Umoja wa Mataifa aliliambia Baraza la Usalama kwamba licha ya nchi yake kushukuru kwa msaada wa Umoja huo, lakini ina haki ya kuheshimiwa masuala yake ya ndani.

Umoja wa Mataifa hauzungumzii zaidi juu ya mtafaruku huo. Naibu msemaji Farhan Haq amesema jumuiya hiyo ya kimataifa bado inatafuta ufafanuzi zaidi juu ya jambo hilo, lakini Balozi Haysom anaendelea kuungwa mkono na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, tangu alipomchagua mnamo mwezi Septemba mwaka uliopita kama mwakilishi maalum wa Somalia.

Haysom mwenyewe hazungumzii moja kwa moja kufukuzwa kwake lakini wakati anaposifia maendeleo ya Somalia katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na mipango ya usalama, amesema mivutano ya kisiasa inayoendelea nchini Somalia inaweza kuitumbukiza nchi hiyo kwenye mashaka, akitoa mfano wa kukamatwa kwa Mukhtar Robow na nguvu zilizotumika.

Mwanadiplomasia Nicholas Haysom
Mwanadiplomasia Nicholas Haysom Picha: imago/Xinhua

Alisema maandamano yaliyofuatia baada ya kukamatwa Robow si mfano mzuri kwa uchaguzi ujao. Mwanadiplomasia huyo aliongeza kusema kwamba hatua hiyo inaweza kuchochea uwezekano wa kurudi kwenye makundi yenye msimamo mkali watu waliojitoa kwenye makundi hayo kwa kuzingatia kuacha vurugu  kwa ajili ya kutekeleza mabadiliko ya kisiasa.

Balozi wa Somalia katika Umoja wa Mataifa, Abukar Dahir Osman, alisema taifa lake linakubali usaidizi mkubwa wa Umoja wa Mataifa lakini unapaswa kunatofautisha kati ya taasisi zake na mwenendo wa watu binafsi ulio na athari mbaya kwa taifa hilo tete.

Balozi huyo alisema kwamba Robow, ambaye alikamatwa siku chache kabla ya uchaguzi wa Desemba mwaka jana, alikuwa mgombea anayeongoza kwenye uchaguzi huo wa urais lakini hakuweza kugombea kwa sababu hakuwa amekamilisha taratibu za kujiondoa kwake kwenye kundi la kigaidi. 

Robow, naibu wa zamani wa kiongozi wa  kundi la al-Shabab lenye mafungamano na kundi la kigaidi la al-Qaida, alijitoa kutoka kwenye kundi hilo mnamo mwaka 2017 na kujisalimisha kwa serikali, ambayo ilifurahishwa na hatua yaake hiyo.

Lakini alipokamatwa, wizara ya usalama ya Somalia ilisema Robow alishindwa kuikana itikadi kali na inamlaumu kwa kuendelea kuhamasisha makundi yenye silaha.

Serikali ya Somalia ilimwamuru Haysom, mwanasheria kutoka Afrika Kusini na mwanadiplomasia mwenye uzoefu, kuondoka nchini humo siku ya Jumanne (Januari 2), baada ya kuandika barua ya kutaka maelezo kuambatana na msingi wa kisheria juu ya kukamatwa kwa Robow, ambaye alikuwa mgombea wa urais wa jimbo la Kusini Magharibi mwa Somalia.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia una jukumu la kusaidia juhudi za amani na kuimarisha taasisi za serikali katika taifa hilo la Pembe ya Afrika, ambalo limeharibiwa kufuatia miongo kadhaa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Mwandishi: Zainab Aziz/APE/AFPE

Mhariri: Mohammed Khelef