1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kura ya kujitenga yaungwa mkono Katalonia

Saumu Mwasimba
2 Oktoba 2017

Vurugu kubwa zimeugubika mchakato wa kura ya maoni ya kujitenga kwa jimbo lenye utajiri mkubwa nchini Uhispania

https://p.dw.com/p/2l5fY
Spanien Madrid Demonstration für Einheit Spaniens
Picha: Reuters/R. Marchante

Maafisa wa jimbo lenye utawala wake wa ndani nchini Uhispania la Katalonia wametangaza ushindi wa kura ya ndio katika mchakato wa kura ya maoni ya kutaka kujitenga na nchi hiyo. Matokeo ya mwanzo yaliyotangazwa leo Jumatatu yanaonesha kwamba wakatalonia waliowengi wamepiga kura kuunga mkono kujitenga. Zoezi la kura ya maoni liligubikwa na vurugu kubwa pamoja na matumizi ya nguvu za vyombo vya usalama kupita kiasi ambapo watu chungunzima wameripotiwa kujeruhiwa wakiwemo polisi pia.

Msemaji wa serikali ya jimbo la Katalonia Jordi Turull amewaambia waandishi habari jana usiku kwamba asilimia tisini ya wakatalonia milioni 2.26  waliopiga kura jana jumapili walipiga kura ya ndio inayomaanisha wanaunga mkono kujitenga na Uhispania.Kiasi asilimi 8 ya wapiga kura walipigakura ya hapana wakati kura nyingine zilizobakia ni za wale walioamua kutounga mkono upande wowote kwa maneno mengine zilikuwa ni kura za maruhani.Turull aliongeza kusema kwamba kuna kura nyingine 15,000 ambazo bado zilikuwa zikihesabiwa huku pia akieleza kwamba idadi hiyo ya kura haijumuishi zile ambazo zimechukuliwa kwa nguvu na polisi wa Uhispania  wakati zilipozuka vurugu kufuatia polisi hao kutaka kuzuia kura hiyo ya maoni isifanyike.

Spanien Katalonien Unabhängigkeits-Referendum - Fernsehansprache von Rajoy
Waziri mkuu wa Uhispania-Mariano RajoyPicha: Getty Images/AFP/J. Soriano

Mahakama ya Uhispania ilipiga marufuku kufanyika kwa zoezi hilo na kuamuru polisi kuzuia lisiendelee na hapo ndipo zilipotokea vurugu kubwa ambapo kiasi watu 844 na askari 33 walijeruhiwa katika uvamizi huo wa polisi.Waziri mkuu wa Uhispania Mariano Rahoj sasa anakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kikatiba ambao haujapata kuikumba nchi hiyo kwa miongo kadhaa kutokana na kura hiyo ya maoni iliyoungwa mkono na wakatalonia waliowengi kufungua njia kwa jimbo hilo lenye utajiri mkubwa kuelekea katika hatua kamili ya kujitenga.Waziri mkuu huyo wa Uhispania akionekana mtu aliyevunjwa moyo amesema kura ya kujitenga ya wakatalonia haina matokeo mazuri isipokuwa imesababisha tu kuzidisha mtengano.

''Mchakato huu wa kura ya maoni umeshindwa.Umefanikiwa tu kuongeza mtengano,mapambano ya raia,vurugu mitaani na kusababisha hali isiyokubalika.Imechangia tu kusababisha madhara katika ushirikiano wetu.ushirikiano ni kitu kizuri ambacho tunapaswa kuanza kukitafuta tena haraka iwezekanavyo.Nasema wazi sitofunga mlango wowote,sijawahi kufanya hivyo.hivyo sivyo ninavyoendesha siasa zangu.Siku zote nimekuwa mweli na muwazi katika majadiliano lakini siku zote nazingatia sheria na siku zote nazingatia demokrasia.''

Spanien Referendum Katalonien Carles Puigdemont
Rais wa Katalonia Carles PuigdemontPicha: Getty Images/D. Ramos

Jumatatu  (02.10.2017) mitaa ya mji wa Barcelona,mji mkuu wa jimbo la Katalonia ilikuwa kimya kabisa ingawa magazeti yameandika kwamba  kura ya maoni iliyopigwa marufuku na serikali kuu mjini Madrid na  ambayo imeungwa mkono na wakatalonia asilimia 90 imetoa nafasi ya kuanza mvutano na mapambano ya kutolewa uamuzi kati ya serikali ya mjini Madrid na jimbo hilo Gazeti jingine la msimamo wa wastani la jimbo la Katalonia La Vanguardia limeandika kwamba sasa jimbo hilo linaingia katika awamu ya migomo na maandamano ya mitaani sambamba na harakati zaidi na ukandamizaji pia. Waziri wa mambo ya nje wa Katalonia Raul Romeva anasema wakaazi wa jimbo hilo wameudhihirishia ulimwengu uamuzi wao.

''leo hii ulimwengu mzima umejionea kwamba upande mmoja tunakabiliwa na vurugu na aibu,na upande wa pili kuna demokrasia na hadhi.Hili ni zoezi rahisi na zaidi ya hilo hii ni kura tuliyoiomba kuifanya katika taasisi za Umoja wa Ulaya na kutoka serikalini na nchi nyinginezo ambazo zinataka,zinngepelea kufanya na kuitisha kura hiyo kuwa na uwezo wa kujenga dunia ya demokrasia ya uwazi zaidi''

Baraza la mawaziri la jimbo hilo la Katalonia litakutana leo kujadili hatua inayofuata baada ya kura hiyo.Kiongozi wa jimbo hilo   jana alitangaza kwamba wapiga kura wa jimbo hilo lenye utawala wake wa ndani wanahaki ya kupata uhuru wao na akaweka wazi kwamba atawasilisha matokeo ya kura hiyo ya maoni mbele ya bunge la jimbo hilo ambalo lina haki ya kuusukuma mbele muswaada wa kutaka uhuru wa jimbo hilo.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman