1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakazi katika miji inayozingirwa nchini Syria kuhamishwa

Isaac Gamba
29 Machi 2017

 Wakazi wa kisuni katika miji miwili inayozingirwa na serikali ya Syria watahamishwa ili kwa upande mwingine waweze kuhamishwa wakazi wa kishia na familia zao kutoka miji miwili inayozungukwa na upinzani.

https://p.dw.com/p/2aDAE
Syrien-Krieg Streitkräfte des Regimes führen Luftangriffe in Hamuriye, Ost-Ghouta
Picha: picture-alliance/abaca/S. Tatin

Miji miwili yenye idadi kubwa ya washia ya al-Foua na Kefraya katika jimbo la kaskazini mashariki la Idlib yenye mafungamano na serikali imezingirwa na wapiganaji wa makundi ya waasi wakati miji inayodhibitiwa na makundi ya waasi ya Zebadani na Madaya iliyoko karibu na mpaka wa Lebanon imezingirwa na vikosi vinavyoiunga mkono serikali.

Mkuu wa shirika hilo la waangalizi wa haki za binadamu nchini Syria Rami Abdel Rahman  amesema zoezi la kuwaondoa watu katika miji hiyo halitaanza hadi April 4 lakini usitishwaji mapigano katika miji hiyo ulianza usiku wa kuamkia leo na kuwa hali hivi sasa ni shwari katika maeneo hayo.

Miji hiyo minne ni sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa mwaka 2015 ambapo pia chini ya makubaliano hayo mashirika ya misaada yamekuwa yakisambaza mahitaji kwenye miji hiyo.

Serikali ya Syria inayoungwa mkono kijeshi na vikosi vya Urusi na Iran imefikia makubaliano kadhaa yanayoashiria uhakika wa usalama wa njia kwa makundi ya  pande zote mbili yanayohusika na mgogoro huo.

Upinzani nchini Syria wasema hatua hiyo inalenga kuinufaisha zaidi serikali ya Assad

Syrien Präsident Bashar al-Assad
Rais wa Syria Bashar al-AssadPicha: imago/ITAR-TASS

Upinzani nchini Syria unaichukulia hatua hiyo kuwa inalenga kuwaondoa kwa nguvu wapinzani wa  Rais Bashar al-Assad kutoka katika miji ya magharibi mwa Syria ambayo kwa kipindi cha miaka sita ya mgogoro wa Syria imekuwa ni mhimili wa utawala wa Rais Assad.

Duru kutoka vyanzo vyenye mafungamano na serikali zimesema utekelezaji wa hatua ya kuondolewa kwa wakazi katika maeneo hayo yaliyozingirwa ulitarajiwa kuanza Aprili 4, kwa kuwaondoa watu 16,000 wanaoishi katika miji ya al-Foua na Kefraya kwa mabadilishano  na wanamgambo wa Zabadani na Madaya pamoja na familia zao.

Taarifa hizo hazikuthibitishwa na upande wa upinzani.

Shirika la waangalizi wa haki za binadamu limesema zoezi la kuwaondoa watu kutoka   miji ya al-Foua na Kefraya limepangwa kuchukua muda wa siku 60 na kuwa watu watakaoondolewa kwenye miji  inayodhibitiwa na waasi watapelekwa Syria Kaskazini.

Makubaliano hayo pia yanahusisha usitishaji mapigano katika maeneo yanayozunguka kusini mwa Damascus pamoja na usambazaji wa misaada ya kiutu na kuachiwa kwa wafungwa 1,500 wanaoshikiliwa  na serikali wakihusishwa na vuguvugu la uasi dhidi ya utawala wa Rais Assad.

Zaidi ya watu 320,000 wameuawa na mamilioni zaidi wamelazimika kuyahama makazi yao tangu mgogoro huo wa Syria ulipoibuka mnamo Machi 2011.

Mwandishi: Isaac Gamba/ RTRE/AFPE

Mhariri: Gakuba, Daniel