1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakenya milioni 1.4 wakabiliwa na njaa

Admin.WagnerD19 Aprili 2021

Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Kenya limesema zaidi ya Wakenya milioni 1.4 wanakabiliwa na baa la njaa na wanahitaji msaada wa dharura.

https://p.dw.com/p/3sDKN
Kenia Athi-Fluss
Picha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Zaidi ya Wakenya milioni 1.4 wanakabiliwa na baa la njaa na wanahitaji msaada wa dharura. Shirika la msalaba mwekundu nchini humo limesema maeneo yaliyo kwenye hatari ya janga hilo pia yanakabiliwa na mizozo ya kiusalama na kuibua wasiwasi wa kutokea mapigano wakati jamii zinapowania rasilimali finyu zilizopo. 

Sikiliza Zaidi: 

Je, Kenya itakabiliwa na baa la njaa?

Shirika la msalaba mwekundu nchini Kenya limetangaza kwamba zaidi ya watu milioni 1.4 nchini wanakabiliwa na njaa, watoto laki nne wakikosa lishe bora wanaohitaji usaidizi wa dharura.

Shirika hilo linaeleza kwamba hali ni mbaya zaidi katika kaunti za Turkana, Mandera na Marsabit, kaunti zingine sita ambazo ni Baringo, Wajir, Tana River, Kilifi, Garissa na Isiolo zikionyesha dalili mbaya. Katibu mkuu wa shirika hilo Dakta Asha Mohammed amesema "Hali ya usalama wa chakula imeendelea kudorora katika maeneo kame nchini kuanzia mwisho wa mwaka jana kutokana na kupungua kwa mvua, na jua kali lililoshuhudiwa mwezi Januari na Februari mwaka huu. Hali hii inatarajiwa kuendelea hadi mwezi mei mpaka mwezi Oktoba.”

Kenia Turkana | Unterernährung
Mkazi wa Turkana, eneo ambalo linakabiliwa na kitisho cha njaa na mapigano kutokana na ufinyu wa rasilimaliPicha: DW/S. Wasilwa

Inahofiwa kwamba hali hii huenda ikachochea zaidi ukosefu wa usalama katika maeneo yanayoshuhudia mizozo ya kijamii, wakati jamii zinapong'ang'ania raslimali finyu zinazopatikana.

Siku moja baada ya zaidi ya majambazi 40 kuvamia eneo la Arabal, kaunti ya Baringo na kumuua mtu mmoja kabla ya kutoweka na zaidi ya mifugo 200, serikali ilitangaza kurejelea oparesheni ya kuwasaka majambazi hao katika kaunti za Turkana, Baringo na Laikipia.

Mkuu wa eneo la bonde la ufa George Natembeya amesema kuwa oparesheni hiyo itahusisha upokonyaji wa silaha haramu pamoja na kuidhinishwa kwa amri ya kutotoka nje.

Makala ya Mbiu ya Mnyonge

Hatua hii inakuja baada ya kutibuka kwa majadiliano kati ya viongozi wa maeneo haya na wanajamii, waliopendekeza kusitishwa kwa oparesheni ya polisi kwa siku 30 ili kutoa nafasi kwa muafaka kupatikana kwa njia ya amani.

Kadhalika Shirika la msalaba mwekundu linaeleza kwamba Wakenya wanakabiliwa na tishio la majanga mawili tofauti yanayotokea wakati mmoja. Huko magharibu mwa Kenya, sehemu zinazopakana na Ziwa Victoria pamoja na baadhi ya maeneo ya bonde la ufa, yanashuhudia makali ya mafuriko.

Shirika hilo linafuatilia hali, ikizingatiwa kuwa familia elfu 11 zilizoachwa bila makao mwaka 2019, bado zinahitaji huduma muhimu za afya, chakula na makao.

Wakio Mbogho, DW, Nakuru.