1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakenya wasubiri tamko la Raila

John Juma
16 Agosti 2017

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga ambaye alishindwa katika uchaguzi wa rais wiki iliyopita anatarajiwa kutoa tamko lake leo kuhusu hatua atakayochukua kuhusiana na madai kuwa ushindi wake uliibwa.

https://p.dw.com/p/2iJLK
Kenia Raila Odinga PK in Nairobi
Picha: Reuters/B. Ratner

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga ambaye alishindwa katika uchaguzi wa rais wiki iliyopita anatarajiwa kutoa tamko lake leo kuhusu hatua atakayochukua kuhuasiana na madai kuwa ushindi wake uliibwa. Kando na hayo, serikali imesitisha hatua ya msako dhidi ya shirika la kutetea demokrasia hadi uchunguzi ufanyike. Shirika hilo liliibua maswali kuhusu uhuru na uwazi katika uchaguzi uliopita.

Wakenya wanasubiri leo hii tangazo la Raila Odinga kuhusu mwelekeo atakaochukua kuhusu madai yake kuwa uchaguzi wa wiki iliyopita ulikumbwa na udanganyifu na kuwa ushindi wake uliibiwa. Rais Uhuru Kenyatta alitangazwa mshindi wa urais.

Tamko la Raila kutuliza taharuki?

Maafisa wa polisi wakiwakabili waandamanaji eneo la Mathare Nairobi
Maafisa wa polisi wakiwakabili waandamanaji eneo la Mathare NairobiPicha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Raila alitarajiwa kutoa tamko lake jana Jumanne, lakini akaahirisha kufuatia kile timu yake ilisema ni shughuli nyingi za kuhakiki fomu za uchaguzi na majadiliano marefu kati yake na vinara wengine wa muungano wa upinzani NASA.

Hata hivyo kauli yake kuwa hakuna kurudi nyuma na matamshi ya maafisa wengine wa muungano wa NASA kuwa mahakama si njia mbadala ya kutafuta suluhisho dhidi ya madai yao, zimezidi kuibua taharuki nchini humo, huku kukiwa na hofu ya kuzuka kwa vurugu zaidi.

Watu 17 wamefariki akiwemo mtoto wa miezi 6 na msichana wa miaka minane waliopigwa na polisi tangu ghasia zilizofungamana na uchaguzi huo kuanza wiki iliyopita. Jamii ya kimataifa, ikiwemo Umoja wa Mataifa na watu wengine nchini Kenya wamemshauri Raila Odinga kutumia njia za kisheria katika kuyashughulikia malalamiko yake.

Raila, mwenye umri wa miaka 72, ni mwanasiasa wa muda mrefu na sasa amepoteza kinyang'anyiro cha urais mara nne.

Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto
Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William RutoPicha: Reuters/T. Mukoya

Misako dhidi ya shirika la AFRICOG

Kando na hayo, polisi na maafisa wa kodi nchini Kenya mapema leo walivamia ofisi za shirika linalotetea demokrasia la AFRICOG, ambalo liliwahi kuibua maswali kuhusu uhuru na haki katika uchaguzi huo wa wiki jana.

Runinga za Kenya zimeonesha picha za maafisa hao katika msako huo, unaofuatia barua za serikali hapo jana zinazolilaumu shirika hilo na pamoja na Tume ya Kutetea Haki za Binadamu nchini humo, KHRC, kwa ukwepaji kodi.

Misako yasitishwa

Hata hivyo muda mchache baadaye waziri wa usalama wa ndani, Fred Matiang'i, ameagiza kuwa misako hiyo isimamishwe hadi uchunguzi ufanywe.

Kamishna Roselyn Akombe(wa tatu kutoka kulia) kwenye picha
Kamishna Roselyn Akombe(wa tatu kutoka kulia) kwenye pichaPicha: DW

Matiang'i amemuandikia barua mkurugenzi mkuu wa bodi inayosimamia mashirika yasiyo ya serikali nchini humo, Fazul Mohamed, kusitisha hatua za kuyaondoa mashirika hayo kwenye usajili au misako dhidi yao hadi wizara ya usalama ifanye uchunguzi wake.

Afisa wa IEBC azuiliwa kusafiri

Wakati huo huo, maafisa nchini Kenya wamesema kuwa afisa mmoja mkuu wa tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini Kenya amezuiliwa kusafiri kuelekea Marekani katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta.

Tume ya IEBC kupitia ukurasa wao wa Twitter imethibitisha kuwa kamishna wao, Roselyn Akombe, alizuiliwa kidogo na maafisa ambao wameomba msamaha lakini sasa ameruhusiwa kusafiri kushiriki mkutano rasmi na atarejea Jumapili.

Mwandishi: John Juma/AFPE/RTRE/APE

Mhariri: Mohammed Khelef