1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakenya wateua wagombea wa uchaguzi

21 Januari 2013

Uchaguzi wa vyama kuwateua wagombea viti mbalimbali kwenye uchaguzi mkuu wa tarehe 4 mwezi Machi umeanza leo kote nchini huku shughuli hiyo ikianza kuchelewa kutokana na kucheleweshwa kwa makaratasi ya kupigia kura.

https://p.dw.com/p/17La0
uchaguzi wa awali Kenya
uchaguzi wa awali KenyaPicha: DW

Vituo vingi vimefunguiliwa kuchelewa huku wapiga kura wakilalamika kwamba hiyo ni hila ya baadhi ya vyama kutaka kuiba kura. Shughuli hiyo iliyokuwa imepangiwa kuanza saa mbili asubuhi haikuweza kuanza wakati huo huku wapigaji kura wakisongamana katika milango ya vituo kusubiri vituo vifunguliwe. Kuna wengine waliosubiri hadi saa sita mchana kabla shughuli hiyo kuanza.

Huku wengine wakiteta kwamba hiyo ni njama ya baadhi ya vyama kutaka kuiba kura. Wengi waliorauka ni wale wanaofanya kazi katika ofisi mbali mbali waliopanga kupiga kura mapema ili waende kwao makazini.

Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa kwa kuchelewa
Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa kwa kuchelewaPicha: DW

Hakuna taarifa yoyote rasmi ambayo imetolewa kufikia sasaa  kuhusu kuchelewa kwa vifaa vya kupigia kura kutoka kwa vyama vikuu vinavyowasilisha wagombea yaani Muungano wa Jubilee Coalition na ule wa CORD.

Wapiga kura wataka muda uongezwe

Shughuli hiyo ya uteuzi imekuwa mtihani mkubwa kwa vyama vya kisiasa kujitambua  kiwango ambacho vimejiandaa kwa uchaguzi mkuu ujao. Usalama umeimarisha huku idara ya polisi ikiwatuma maafisa 66,000 wa usalama katika vituo 33,000 vya kupigia kura kote nchini. Ingawaje hakuna kisa chochote cha vurugu ambacho kimeshuhudiwa, wasiwasi mkubwa ni wakati wa kutangazwa kwa matokeo baada ya shughili itakapokamilika na kura khesabiwa leo jioni kwani wale watakaoshindwa watakuwa na sababu kwamba uchaguzi haukuwa huru na haki.

Ulinzi ni suala la muhimu katika uchaguzi
Ulinzi ni suala la muhimu katika uchaguziPicha: AP

Tayari baadhi ya wapigaji kura wanataka muda wa kupiga kura uongezwe ili kufidia muda uliopotea. Uteuzi wa leo ni wa wagombea viti vya Ugavana Useneta, Waakilishi wa Wanawake na Madiwani. Tayari vyama vikuu na miungano ya kisiasa imewatangaza wagombea urais na manaibu wao kupitia makubaliano ya vyama tanzu na uteuzi wa wajumbe.

Vyama vyote vya kisiasa vilitakiwa kuandaa uteuzi wao wakati mmoja ili kuwazuia wagombea wanaoshindwa kuhamia vyama vingine.

Mwandishi: Alfred Kiti

Mhariri: Josephat Charo