1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yatarajia wakimbizi 60,000 kutoka Syria

6 Februari 2016

Maelfu ya Wasyria wanateseka kutokana na baridi kali na mvua katika mpaka wa Uturuki baada ya kuikimbia harakati ya jeshi la serikali dhidi ya mji wa Aleppo inayoungwa mkono na Urusi kaskazini mwa Syria.

https://p.dw.com/p/1HqtZ
Syrer flüchten Richtung türkische Grenze
Picha: picture alliance/AP Photo

Maelfu ya raia wameyakimbia mapigano makali wakati wanajeshi wa serikali wakisonga mbele wiki hii dhidi ya waasi, wakifaulu kuifunga njia muhimu ya kupitishia mahitaji inayoelekea Aleppo. Operesheni hiyo imezua hatari ya kutokea janga jipya la kibinaadamu.

Mapema leo kivuko cha mpaka wa Uturuki cha Oncupinar, kinachopakana na Bab al-Salama upande wa Syria, kimebakia kufungwa, huku maafisa wa Uturuki wakisema wanajaribu kutengeneza nafasi katika kambi zilizopo kuwapa hifadhi wakimbizi wanaowasili.

"Timu zetu ziko tayari kuwapa maji na chakula mara tu watakapowasili," alisema mkuu wa Shirika la hilali nyekundu la Uturuki, Ahmet Lutfi Akar.

Kwa mujibu wa shirika la haki za binaadamu la Syria, takriban raia 40,000 wameyahama makazi yao kuikimbia operesheni ya serikali. "Hali ya watu walioyakimbia makazi yao ni mbaya," amesema Rami Abdel Rahman, Mkurugenzi wa shirika hilo lenye makao yake makuu mjini London, Uingereza. "Familia zimekuwa zikilala nje kwenye baridi katika viwanja na mahema bila kuwepo asasi za kimataifa zisizo za serikali kuwasaidia.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu alisisitiza kwamba nchi yake itaendelea kuitumia sera yake ya mipaka wazi kwa wakimbizi kutoka Syria. "Tunaendelea kuitumia sera hii ya mipaka wazi kwa watu hawa wanaokimbia uvamizi, utawala pamoja na mashambulizi ya kutokea angani ya Urusi," alisema.

Türkischer Außenminister Cavusoglu
Mevlut Cavusoglu, waziri wa mambo ya nje wa UturukiPicha: AFP/Getty Images/A. Altan

"Tayari tumewapokea Wasyria 5,000; wengine 50,000 hadi 55,000 wako njiani na hatuwezi kuwaacha hapo," aliongeza kusema.

Awali maafisa wa Umoja wa Ulaya waliikumbusha Uturuki kuhusu majukumu yake ya kimataifa kuiweka mipaka yake wazi kwa wakimbizi. "Mkataba wa Geneva bado unatumika unaosema sharti uwachukue wakimbizi," alisema kamishna wa Umoja wa Ulaya anayehusika na upanuzi na sera ya kikanda, Johannes Han.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu misaada ya kibinadamu OCHA imekadiria kwamba hadi watu 20,000 wamekusanyika katika kivuko cha Bab al-Salama na wengine 5,000 hadi 10,000 wamekimbilia katika mji ulio karibu wa Azaz. Tayari Wasyira kati ya milioni 2 na 2.5 wanaioshi nchini Uturuki baada ya kukimbia mzozo nchini mwao uliodumu miaka mitano sasa.

Syria yaonya dhidi ya harakati ya kijeshi ya ardhini

Wakati haya yakiarifiwa, serikali ya Syria kwa upande wake imeonya itapambana vikali na wanajeshi wowote wa ardhini watakaotumwa nchini humo, kufuatia ripoti kwamba Saudi Arabia na Uturuki zinazowasaidia wapiganaji waasi, huenda zikatuma wanajeshi.

Walid Muallem Syrien Außenminister
Walid Muallem, waziri wa mambo ya nje wa SyriaPicha: picture-alliance/dpa

"Harakati yoyote ya ardhini nchini Syria bila idhini ya serikali itakuwa ni uvamizi ambao lazima ukabiliwe," alisema waziri wa mambo ya nje wa Syria, Walid Muallem, katika mkutano na waandishi wa habari mjini Damascus.

"Mtu yeyote asifikirie anaweza kuishambulia Syria au kukiuka uhuru wake kwa sababu nawahakikishia mvamizi yeyote atarejea nchini mwake katika jeneza la mbao, awe ni raia wa Saudi Arabia au Mturuki," alionya.

Alhamisi iliyopita Saudi Arabia iliacha wazi uwezekano wa kutuma wanajeshi, ikijitolea kutuma vikosi kama muungano unaoongozwa na Marekani dhidi ya wapiganaji wa jihad wa kundi la dola la kiislamu utaamua kufanya operesheni ya ardhini.

Na Urusi, ambayo pamoja na hasimu wa Saudia Arabia katika kanda hiyo, Iran, imeishutumu Uturuki kwa maandalizi ya uvamizi wa kijeshi nchini Syria, madai ambayo serikali ya mjini Ankara imeyapuuzilia mbali.

Mwandishi:Josephat Charo/afpe/dpae

Mhariri:Sudi Mnette