1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakinamama watumiliwa nguvu Sierra Leone

Mohamed Dahman24 Novemba 2009

Jinsi wakinamama wanavyodhalilishwa ulimwenguni-tuchukue mfano wa Sierra Leone

https://p.dw.com/p/KeRb
Wanafunzi nchini Sierra LeonePicha: DW/Schaeffer

Mwanamke mmoja katika kila kundi la wanawake watatu duniani huwa amepigwa, amelazimishwa kufanya mapenzi au kudhulumiwa katika maisha yake.Wakati wa vita na wakati wa amani wanawake wanaendelea kuteseka.Vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake vimeenea barani Afrika.Sierra Leone ilioko Afrika Magharibi ni nchi ambayo ukatili dhidi ya wanawake ulikuwa umetapakaa wakati wa vita ambavyo vimemalizika karibu miaka tisa iliopita.Hata hivyo licha ya kumalizika kwa vita hivyo wanawake wengi nchini Sierra Leone wanaendelea kukabiliana na ukatili wa aina fulani kila siku.

_________________________

Vita vimemalizika lakini bado kuna kiwango kikubwa cha ukatili dhidi ya wanawake nchini Sierra Leone.Wakati wa muongo mzima wa vita nchini humo wanawake na wasichana walibakwa,walilazimishwa kufunga ndoa, walishambuliwa na walitumiwa kama watumwa wa ngono-Patricia George ni mmojawapo wa wanawake hao. Alikuwa na umri wa miaka kumi tu wakati alipotekwa hapo mwaka 1991 na waasi wa kundi la Revolutionary United Front (RUF).

' Nilitekwa na muasi na kupelekwa kichakani ambapo nilitolewa bikira na baadae kuja kijifunguwa watotio wawili. Kwa miaka kumi nilikaa na mwanaume huyo muasi.Alikuwa akinipiga,akinibaka na kutishia kuniuwa iwapo sitamruhusu kuugusa mwili wangu. Alinitumia na kunidhulumu miaka yote hiyo.'

Patricia ni miongoni ma maelfu ya wanawake na wasichana ambao wamevunjiwa haki zao wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sierra Leone.Hata hivyo hata baada ya kumalizika kwa vita wanawake nchini humo wanaendelea kukabiliana na vitendo vya ukatili.Juu ya kwamba Patricia alimkimbia muasi aliekuwa akimshikilia kabla ,rafiki yake mpya aliempata baada ya vita hakuwa bora kuliko muasi aliekuwa naye kabla.

'Mwanaume huyo mwengine niliekuwa naye alikuwa pia akinipiga.Nilidhani atakuwa msaada kwangu baada ya kuteseka sana lakini alinitesa na aliniacha kwa sababu alisema sikwenda shule.Vipi ningeliweza kwenda shule ...kwa miaka kumi nilikuwa kichakani.Ilinibidi niwahudumie watoto wangu na ili kuweza kuendelea kuishi nimekuja kuwa kahaba.'

Lakini hivi sasa Patricia anauangalia mustakbali kwa matumaini.Alimepatiwa mafunzo ya kusuka nywele na shirika lisilo la kiserikali la Wanawake katika Mizozo.

Shirika hilo lililoanzishwa hapo mwaka 1997 linatowa ushauri nasaha na kuwapa mafunzo zaidi ya wanawake na wasichana mia mbili ambao wamekumbwa na aina fulani ya ukatili wakati na baada ya vita. Juliana Conteh Mkurugenzi wa shirika hilo la Women in Crisis anasema wanawake ambao wamedhalilishwa nchini Sierra Leone mara nyingi hubakia kimya kwa kuona aibu na kushindwa kushughulikia vitendo vya ukatili wa kijinsia. Anasema kunahitajika kuchukuliwa hatua zaidi ili kazi hiyo iweze kufanya kazi ipasvyo.

' Serikali inatakiwa isaidie watowa huduma na wahanga. Mawakili na watowa huduma wanatakiwa wapatiwe rasilmali ili kwamba wawe na furaha kufanya kazi hiyo.Na kwa wahanga wanahitaji kweli kupatiwa rasilmali kwa ajili ya kuwawezesha.Pia tunahitaji kuwahusisha wanaume katika kupanga na kutekeleza mchakato wa harakati za vitendo vya ukatili vinvyofanywa chini ya misingi ya kijinsia.Na wale wanaohusika na dhuluma hizo lazima waadhibiwe.'

Hata hivyi ili wale wanaotenda dhuluma hizo waweze kuadhubiwa wanawake lazima wawe majasiri vya kutosha kuzifikisha kesi hizo mahkamani bila ya kujali aina ya uhusiano ulioko kati yao.naibu inspekta wa upelelezi Mira Koroma ni Naibu mkurugenzi wa kitengo cha kusaidia familia katika Jeshi la Polisi nchini Sierra Leone.Idara hiyo huchunguza na kuendesha kesi za makosa ya ngono na ukatili wa majumbani.Inspekta koroma anasema licha ya kuwepo kwa sheria za jinsia zilizopitishwa hapo mwaka 2007 wanawake wengi nchini humo mara nyingi wana goma kufunguwa kesi za kushambuliwa kwao

'Wanawake wenyewe binafsi hawataki kukubali kwamba ukatili wanofanyiwa ni dhuluma.Kwa mfano wakati mwanamke anapopigwa na mume wake au rafiki yake haoni hilo kuwa ni kosa.Wakati mwanamke anapobakwa na mume wake haoni hilo ni kosa. Kwa hiyo tuna changamoto kwamba hayo ni makosa wanayotendewa na kwamba wanapaswa kuripoti polisi'

Hata hivyo ni jambo la kutia moyo kwamba hivi karibuni mahkama maalum kwa ajili ya Sierra Leone ni mahkama ya kwanza ya kimataifa kutowa hukumu kwamba ndoa za lazima ambazo huhusiha ukatili dhidi ya wanawake wakati wa vita ni uhalifu dhidi ya ubind´naadamu.

Mwandishi:Bomkapre Kamara/Mohamed Dahman

Mhariri:Abdul Rahman