1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakulima wa kahawa Uganda hawapati faida

Josephat Charo10 Septemba 2007

Wakulima wa kahawa nchini Uganda wanateseka kutokana na uhusiano wa kibiashara usio wa haki kati yao na Ulaya, ingawa kahawa yao ni mojawapo ya kahawa bora zaidi duniani. Hayo ni kwa mujibu wa halshauri ya sekta ya kahawa nchini Uganda.

https://p.dw.com/p/CHjP
Kahawa baada ya kuvunwa
Kahawa baada ya kuvunwaPicha: AP

Henry Ngabirano, mkurugenzi wa halmshauri ya kuendeleza kahawa nchini Uganda, anasema wanaopata hasara kubwa ni wakulima wanaohusika moja kwa moja katika uzalishaji wa kahawa. Juu ya hayo, wakulima wa Uganda hawanufaiki vya kutosha kutokana na faida inayotokana na uuzaji wa kahawa.

Kwa pamoja wakulima wa Uganda na wauzaji wa kahawa katika nchi za kigeni hupokea asilimia sita ya bei ya kahawa inayouzwa. Hayo ni kwa mujibu wa halmashauri ya kuendeleza kahawa ya Uganda. Bwana Henry Ngabirano amesema hii inaonyesha kiwango cha unyanyasaji kilichopo.

Kahawa ni zao linaloongoza katika kupata fedha na uzalizaji wake huchangia karibu asilimia 50 ya uchumi wa Uganda. Uganda imekuwa ikiongoza katika uzalishaji wa kahawa aina ya robusta tangu mzozo wa kisiasa ulipozuka nchini Ivory Coast, ambayo ilikuwa ikiongoza katika uzalishaji wa aina hiyo ya kahawa. Wauzaji kahawa katika nchi za kigeni wamesema mapato yao yaliongezeka kwa asilimia 65 kufikia dola milioni 17,9 mnamo mwezi Mei mwaka huu, ikilinganishwa na mwaka jana.

Ukuaji huu ulitokana na bei za juu na watumiaji wa kahawa katika nchi za kaskazini na Asia wakinunua kahawa ya hali ya juu. Nchi za Afrika zimekuwa na bahati ya kuwa na maeneo ya miinuko, mashamba madogo ya kufanyia kilimo cha wastani, pamoja na kilimo ambacho hakitegemei madawa ya kisasa ambacho kimeifanya kahawa kuwa bora na ya kuvutia zaidi katika soko la kimataifa.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa muungano wa kahawa wa Afrika Mashariki, Philip Gitao, kahawa kutoka Afrika bado inahitajika kwa wingi. Aidha mkurugenzi huyo amesema kahawa ya Afrika hutumiwa kuboresha aina mbalimbali za vinjwaji asili na imeendelea kuuzwa peke yake bila kuchanganywa na vitu vingine.

Katika miaka ya 1990 Uganda ilibadili sera yake kuhusu uzalishaji wa kahawa. Soko la kahawa liliwekwa huru na vikwazo kwa wakuzaji kahawa vikaondolewa. Shilingi ya Uganda iliweza kubadilishwa na sarafu nyingine na vikwazo vya kudhibiti bei vikaondolewa. Bwana Henry Ngabirano anasema serikali ya Uganda iliona kahawa ina jukumu katika kuangamiza umaskini. Idadi ya wakulima wa kahawa iliongezeka wakati huo huku Waganda wakiona fursa ya kufanya biashara katika kilimo cha kahawa.

Lakini wakulima wanakabiliwa na changamoto kadhaa, zikiwemo ukosefu wa mikopo katika benki au ruzuku kutoka kwa serikali ili kuwawezesha kuendeleza kilimo cha kahawa. Ronald Buule, mkulima wa kahawa katikati mwa Uganda, anasema anachokosa ni msaada. Buule anasema ingawa wakulima huunda vyama vya ushirika kutafuta bei nzuri kwa kahawa yao kutoka kwa washenga, faida wanayoipata haitoshi kuhakikisha wana kahawa ya kutosha katika maghala yao na vifaa.

Wakulima wanalazimika kufanya kazi nyingi lakini wanapata pesa kidogo. Wakulima wengi wanalazimika kupanda mazao mbalimbali katika mashamba yao kama vile kakao, mihogo, ndizi, machungwa na vanilla na hata kufuga kuku.

Henry Ngabirano amesema ni aibu kwamba kawaha inayouzwa madukani haimilikiwi na kampuni za Uganda, ingawa malighafi inanunuliwa nchini humo. Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, amesema nchi yake itaendelea tu itakapotengeneza bidhaa zake yenyewe badala ya kuuza malighafi.

Bwana Ngabirano ameongeza kusema kwamba mikataba ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya Umoja wa Ulaya na nchi zinazoendelea inatarajiwa kuendelea kuwahujumu wakulima wa kahawa. Mikataba hiyo inazitaka nchi za Afrika, Karibik na Pacific ziruhusu bidhaa za washirika wao wa kibiashara kutoka Umoja wa Ulaya ziuzwe katika masoko yao.