1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakuu wa majeshi, polisi wakutana Kigali

Admin.WagnerD7 Januari 2014

Wakuu wa majeshi na polisi kutoka nchi za Rwanda, Uganda na Kenya wanakutana mjini Kigali wiki moja baada ya nchi hizo kuamua kutumia vitambulisho vya kawaida kusafiria baina yao.

https://p.dw.com/p/1AmeG
Mkuu wa majeshi ya Uganda, Jenerali Katumba Wamala.
Mkuu wa majeshi ya Uganda, Jenerali Katumba Wamala.Picha: Roberto Schmidt/AFP/Getty Images

Kuanzishwa kwa mkakati huo kulizua wasiwasi kwamba huenda hata wahalifu wa usalama wakaitumia nafasi kuhujumu usalama wa mataifa hayo lakini maafisa hao wanasema ni kupitia ushirikiano wa pamoja utakaowasaidia kulikabili tatizo hilo.

Wanajeshi wa kikosi cha dharura cha Afrika Mashariki.
Wanajeshi wa kikosi cha dharura cha Afrika Mashariki.Picha: DW/L. Ndinda

Mkakati wa kuanza kutumia kitambulisho cha kawaida baina ya nchi za Rwanda, Kenya na Uganda ulianza rasmi tarehe mosi mwezi Januari. Nchi hizo zinasema kwamba hali hii itarahisisha mafungamano ya kibiashara na hivyo kuinua kiwango cha ukuaji wa uchumi na maendeleo miongoni mwa nchi hizo.

Hofu ya kuhujumiwa kwa usalama
Baadhi ya wananchi wanaofanya safari kwenye nchi hizo wanasema mpaka sasa wanafurahia kuwepo kwa hali hiyo.

Hata hivyo wakati wananchi wakipongeza hali kuwa shwari, maafisa wa usalama wanaona hali hii kuweza kuwa nafasi bora kwa wahujumu wa usalama kuingilia kati na kutekeleza vitendo vyao vya ughaidi.

Hii ni moja ya sababu ya wakuu wa majeshi na polisi kutoka nchi hizo kukutana Kigali kulijadili suala hilo."Tunataka ngazi zetu za usalama kwenda pamoja ktk kuhakikisha usalama wa raia wetu wote.

Tunataka kuondoa wasiwasi ambao kidogo umeanza kudaiwa na baadhi ya wananchi wetu kwamba kutumia vitambulisho kunaweza kuwa chanzo cha kuhatarisha usalama, kwa hiyo tunataka kuchukua mikakati pamoja," alisema msemaji wa jeshi la Rwanda Brigedia Jenerali Joseph Nzabamwita.

Wanajeshi wa kikosi cha dharura cha Afrika Mashariki.
Wanajeshi wa kikosi cha dharura cha Afrika Mashariki.Picha: DW/L. Ndinda

Haja ya kushirikiana
Mawaziri wa ulinzi katika nchi hizo wanasema usalama wa kudumu ni msingi wa maendeleo ya mataifa hayo na ndiyo maana wanahitaji kushirikiana kuhakikisha usalama huo kwa mstakabari wa nchi zote.

Kuanza kutumiwa kwa vitambulisho badala ya pasi za kusafiria kuliidhinishwa na marais wa Kenya, Uganda na Rwanda kwenye kikao chao cha tarehe 28 Oktoba mwaka jana ambapo vilevile waliridhia kuwepo kwa vikao vya pamoja miongoni mwa maafisa wa usalama wa nchi hizo.

Mwandishi: Syllivanus Karemera/DW Kigali
Mhariri: Mohammed Khelef