1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waliokufa mashambulizi ya Berlin wafikia 12

Mohammed Khelef
20 Desemba 2016

Kwa mujibu wa polisi, hadi sasa watu 12 wameshapoteza maisha yao na wengine 48 ni majeruhi wa kile ambacho kinaonekana kama mashambulizi ya kupangwa dhidi ya soko la Krismasi katika mji mkuu, Berlin. 

https://p.dw.com/p/2UZdd
Deutschland Neun Tote und viele Verletzte auf Berliner Weihnachtsmarkt
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Magari ya kubebea wagonjwa na magari ya polisi yalikimbilia haraka kwenye eneo la tukio, baada ya lori hilo kuparamia kingo za soko kwenye uwanja mashuhuri kwa watalii, sawa na lile tukio la mwezi Julai mjini Nice, Ufaransa, ambapo watu kadhaa waliuawa.

Kupitia msemaji wake, Steffen Seibert, Kansela Angela Merkel alituma haraka ujumbe wa Twitter usemao: "Tunaomboleza vifo na tuna matumaini kuwa watu wengi waliojeruhiwa watapatiwa msaada."

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Ujerumani, Thomas de Maiziere, amekiambia kituo cha televisheni cha ZDF kwamba hawezi kuthibitisha kuwa ni mashambulizi ya kigaidi, lakini kuna mambo mengi yanayooteza kidole kwenye mkasa huo.

Mashahidi wanasimulia hali ya taharuki na khofu, vilio na damu kila mahala, wakati gari hilo likiwakanyaga watu ovyo ovyo. "Nilisikia kelele kubwa, kisha sote tukatulia, halafu ghafla watu wakaanza kwenda kuyaondoa mabaki ya watu, wakijaribu kumsaidia kila aliyekuwepo," alisema raia wa Australia, Trisha O'Neil, ambaye alikuwa mita chache kutoka eneo la mkasa.

Mamlaka hapa Ujerumani zinasema hakukuwa na ishara ya "hali nyengine zaidi ya hatari karibu na uwanja wa Breidscheidplatz" mjini Berlin, ambako mashambulizi hayo yametokea. 

Deutschland Neun Tote und viele Verletzte auf Berliner Weihnachtsmarkt
Lori lililovamia uwanja wa soko la Krismasi na kuuwa watu 12 na kujeruhi wengine 48 mjini Berlin.Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Polisi wanasema kuwa lori hilo lilitembea umbali wa mita 80 kuelekea kwenye soko la Krismasi kabla ya kusimama.

Mshukiwa atiwa nguvuni

Msemaji wa polisi ya Ujerumani ameliambia shirika la habari la AFP wanamshikilia dereva wa lori hilo, ambaye hadi sasa hawajataja utambulisho wake, huku mwenzake akiripotiwa kufa kwenye mkasa huo.

Hata hivyo, shirika la habari la Ujerumani, dpa, limevinukuu vyanzo vya usalama vikimtaja dereva wa gari hilo kuwa ni muomba hifadhi mwenye asili ya ama Afghanistan au Pakistan, aliyewasili Ujerumani mwezi Februari mwaka huu.

Gazeti la kila siku la Tagespiegel linasema mtu huyo alikuwa anafahamika polisi kutokana na rikodi yake ya uhalifu mdogo mdogo, lakini hakuwa akihusishwa na ugaidi.

Mmiliki wa lori hilo, raia wa Poland, alithibitisha kuwa dereva wake mmoja hajulikani alipo. "Hatujasikia habari zake tangu jioni. Hatujui kilichomtokea. Ni binami yangu, nimemfahamu tangu akiwa mtoto", alisema mmiliki wa kampuni ya usafirishaji, Ariel Zurawski, wakati akizungumza na shirika la habari la AFP.

Ulaya kwenye mashambulizi

Deutschland Neun Tote und viele Verletzte auf Berliner Weihnachtsmarkt
Vikosi vya usalama vikiimarisha doria baada ya mashambulizi mjini Berlin.Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Kiasili, masoko ya Krismasi ni maarufu sana katika miji mikubwa na midogo nchini Ujeurmani na mara kwa mara yamekuwa yakitajwa na vyombo vya usalama kuwa yako hatarini kushambuliwa. 

Mkasa huu wa mara hii umetokea karibu sana na Kanisa la Kumbukumbu ya Mfalme Wilhelm, ambalo liliharibiwa vibaya na mabomu ya Vita Vikuu vya Pili na limehifadhiwa kama ishara ya kuvionya vizazi vijavyo juu ya athari za vita na mashambulizi.

Kwa ujumla, Ulaya imekuwa kwenye hali ya tahadhari kwa kiwango cha juu kwenye mwaka huu wa 2016 unaomalizika, huku mashambulizi yakiikumba zaidi miji ya Paris na Brussels, nayo Ujerumani ikiwa imeshambuliwa mara kadhaa yanayodaiwa kupangwa na kundi lijiitalo Dola la Kiislamu (IS) na kufanywa na waomba hifadhi.

Mwezi Julai, kijana wa Kiafghani aliwashambulia watu kwa shoka ndani ya treni katika jimbo la kusini la Bavaria, ambapo watu watano waliuawa, huku mshambuliaji wa kujitoa muhanga akiwajeruhi wengine 15 ndani ya siku sita kwenye jimbo hilo hilo.

Mwezi Februari, mvulana wa Kijerumani mwenye asili ya Morocco alimchoma kisu na kumjeruhi askari polisi mmoja, naye pia akidai kuitumikia IS.

Kuwasili kwa wakimbizi 890,000 mwaka jana kuliingiza Ujerumani kwenye mzozo mkubwa wa kisiasa, huku wakosoaji wakisema mmiminiko huo ni hatari kwa usalama.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/AFP
Mhariri: Sylvia Mwehozi