1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanafunzi wa vyuo vikuu Algeria wapewa likizo ya mapema

Zainab Aziz Mhariri: Bruce Amani
10 Machi 2019

Wizara ya elimu ya juu nchini Algeria imeamuru likizo ya mapema kwa wanafunzi wa vyuo vikuu katika hatua ya kujaribu kuyadhoofisha maandamano ya kumpinga Rais Abdelaziz Bouteflika kugombea muhula wa tano.

https://p.dw.com/p/3EjSJ
Algerien Präsidentschaftswahlen l Proteste
Picha: picture alliance/NurPhoto/B. Bensalem

Wizara ya elimu ya juu imetangaza kwamba likizo hiyo ya mapema itaanza leo Jumapili na kuendelea hadi Aprili 4. Kwa kawaida likizo hiyo huwa ya wiki mbili na huanza tarehe 21 mwezi Machi hadi Aprili 5 kila mwaka. Walimu na wanafunzi kutoka kwenye vyuo vikuu kadhaa wameanza mgomo, huku wengine wakiahidi kuanza mgomo leo hii Jumapili. 

Rais Bouteflika ambaye ni nadra kuonekana hadharani tangu augue kiharusi mnamo mwaka 2013 ameahidi kutokamilisha muhula wake iwapo atchaguliwa tena katika uchaguzi wa Aprili 18, lakini wanafunzi wa vyuo vikuu wanaipinga hatua hiyo. Uamuzi huo wa Wizara ya Elimu ya Juu umefikiwa baada ya maelfu ya watu kuandamana katikati ya mji mkuu Algiers kwenye maandamano makubwa yaliyowahi kutokea kwenye mji huo mkuu katika kipindi cha miaka 28 kupinga utawala wa miaka 20 wa kiongozi huyo wa zamani.

Maelfu ya wanafunzi wameshiriki kwenye maandamano ya kumpinga Bouteflika tangu kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 82 alipotangaza nia yake ya kugombea muhula wa tano katika uchaguzi wa Urais unaotarajiwa kufanyika April 18.

Katibu mkuu wa wizara ya elimu ya juu nchini Algeria, Abdelhafid Milat, ameukosoa uamuzi wa kutangaza mapema likizo hiyo kwa wanafunzi wa chuo kikuu kabla ya wakati wake. Ameliambia shirika la habari la Ujerumani dpa kwamba ni jambo la kushangaza katika historia ya elimu ya juu nchini Algeria. Milat amesema jumuiya ya elimu ya juu itakutana na kuamua juu ya majibu kufuatia hatua hiyo ya wizara ya elimu ya juu. Maandamano hayo yamekuwa ya amani tangu yalipoanza zaidi ya wiki mbili zilizopita katika nchi hiyo ya Afrika ya Kaskazini.

Polisi wa Algeria wakimbeba mwenazo aliyeumia
Polisi wa Algeria wakimbeba mwenazo aliyeumia Picha: Reuters/Z. Bensemra

Hata hivyo,duru za hospitali ya Mustapha Pacha zimesema raia zaidi ya 100 walijeruhiwa wakati walipopambana na maafisa wa usalama katika mji mkuu wa Algeria, Algiers kwenye maandamano ya siku ya Ijumaa. Baadhi ya waandamanji walijeruhiwa kwa kupigwa mawe na risasi za mpira wakati wengine walipata majeraha kutokana na kupuliziwa gesi ya kutoa machozi na vikosi vya usalama,

Taarifa zaidi zinafahamisha kwamba waandamanaji waliyavamaia makumbusho ya vitu vya kale mjini Algiers mnamo siku ya Ijumaa na Televisheni ya serikali imeripoti juu ya kuzuka kwa moto ndani ya jengo yaliyopo makumbusho hayo na pia kuibiwa baadhi ya vitu vya kale.

Kwa mujibu wa taarifa ya idara ya Usalama wa Taifa, watu wapatao 195 wamezuiwa na kwamba maafisa wa polisi 112 walijeruhiwa kwenye wa maandamano hayo. Rais Bouteflika, ameonya juu ya kutokea machafuko ambapo ameyalaumu makundi kutoka nje ambayo amesema yanataka kuyatumia maandamno hayo kuvuruga amani nchini Algeria.

Bouteflika alinusurika vuguvugu la kupinga serikali lililoanzia katika nchi jirani ya Tunisia mnamo mwaka 2010. Wakati huo, serikali yake ilifaulu kuyazima maandamano ya kuunga mkono demokrasia kwa kutoa ahadi za kufanya mageuzi na kuongeza mishahara kwa kutumia mapato ya nchi yanayotokana na mafuta na gesi.

Katika miaka ya hivi karibuni, uchumi wa Algeria umedorora kutokana na kuanguka bei ya mafuta katika soko la kimataifa hali ambayo imesababisha kupungua kwa ruzuku zinazotolewa na serikali kwa wananchi wake.

Vyanzo: Dpa/AFPE