1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi, waasi wa Congo watuhumiwa kwa uhalifu wa kivita

Josephat Charo
27 Juni 2018

Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wamewatuhumu maafisa wa vyombo vya usalama na wapiganaji wa makundi ya waasi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa kufanya uhalifu dhidi ya ubinadamu katika jimbo la Kasai.

https://p.dw.com/p/30NH7
Demokratische Republik Kongo Beni
Picha: Alain Wandimoyi/AFP/Getty Images

Tuhuma hizo zilitolewa kufuatia uchunguzi ulioanzishwa na baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa mwaka uliopita kuchunguza vitendo vya ukiukaji wa haki huko Kasai, eneo ambalo lilitumbukia katika machafuko mwezi Septemba mwaka 2016, baada ya vikosi vya serikali kumuua chifu wa eneo hilo, Kamwina Nsapu. Chifu huyo alikuwa mpinzani wa serikali ya mjini Kinshasa na sasa waasi wanaopigana kwa jina lake wanapambana na majeshi ya serikali na kundi moja la waasi lilanoegemea upande wa serikali la Bana Mura.

Wachunguzi walisema baadhi ya ukiukaji ulifoanywa na wanajeshi na maafisa wa vikosi vya usalama, kundi la waasi la Bana Mura na kundi la Kamwina Nsapu, ni uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita.

Katika ripoti hiyo itakayowasilishwa kwa baraza la haki za binadamu mwezi ujao, wachunguzi waliwatuhumu wanajeshi wa serikali na wanachama wa makundi ya waasi kwa kuwalenga raia katika mashambulizi yao katika mfumo ulioratibiwa na katika eneo pana, na kuangazia vitendo vya kinyama vikiwemo mauaji, ukataji wa viungo, ubakaji, utumwa wa ngono na vitendo vingine vinavyoishusha hadhi na heshima ya binadamu.

Wachungizi wa Umoja wa Mataifa ambao waliruhusiwa kulitembelea eneo la Kasai kufanya uchunguzi, walisema kuna tatizo sugu la watu kufanya makosa bila kuwa na hofu ya kuchukuliwa hatua yoyote kisheria, ikizingatiwa ukubwa na uzito wa vitendo vya uhalifu vilivyofanywa.

Mkuu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Akage, Access to Justice, mjini Kinshasa, ambalo limekuwa likiwatetea wahanga wa mauaji ya Kasai, George Kapyamba, alisema yaliyotokea Kasai ni mambo mabaya na ameitaka jumuiya ya kimataifa iingilie kati isaidie. "Jumuiya ya kimataifa inatakiwa isimamie haya maneno ya kuwapeleka wale wote waliohusika mbele ya mahakama. Sio korti ya Congo kwa sababu haiwezi kufanya kazi nzuri. Kwa kuwa iko mikononi mwa serikali, haiwezi kufanya haki."

Machafuko yamechochewa kikabila

Ripoti ya wachunguzi wa Umoja wa Mataifa pia ilitambua kwamba machafuko ya Kasai sasa yamegeuka na kuchochewa zaidi na tofauti za kikabila tangu mapema mwaka uliopita. Ripoti ilisema baadhi ya vitendo vya ukiukaji vilivyofanywa na waasi wa kundi la Bana Mura dhidi ya watu wa kabila la Luba na mashambulizi yaliyofanywa na kundi la waasi la Kamwina Nsapu dhidi ya watu wa makabila ya Tshokwe na Pende, yametimiza vigezo vya kuitwa "mateso kwa misingi ya kikabila" na hivyo ni uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Kongo Kananga - Hungersnot: Mütter mit Kindern warten auf Nahrungsmitteln
Akina mama wakiwa na watoto wao wakisubiri chakula huko Kananga, jimboni Kasai.Picha: picture-alliance/dpa/K. Bartlett

Serikali ya Congo kupitia waziri wake anayehusika na masuala ya haki za binadamu, Marie-Ange Mushobekwa, ilisema itatoa taarifa yake kuhusu ripoti hiyo katika mkutano utaofanyika Jumanne wiki ijayo (03.06.2018) mjini Geneva.

Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa waliitaka serikali ya rais Joseph Kabila ifuatilie sera za kuwapokonya silaha mara moja na kuendeleza mchakato wa maridhiano huko Kasai. Lakini kumtaka Kabila autafutie ufumbuzi mzozo wa Kasai huenda kukawa ni kutangwa maji kwenye kinu. Wengi wanamtuhumu Kabila kwa kuongeza changamoto zinazoikabili Congo kwa kukataa kuondoka madarakani wakati muhula wake ulipofika mwisho mwaka 2016.

Wachambuzi walionya kwamba Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo huenda ikapoteza muelekeo na kutumbukia pabaya iwapo Kabila atataka kugombea muhula wa tatu katika uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi Desemba mwaka huu, huku akikaidi sheria ya mihula kwa mujibu wa katiba ya Congo, au iwapo uchaguzi huo utaahirishwa kwa mara ya tatu.

Ripoti hiyo mpya ya Umoja wa Mataifa ilitolewa baada ya maaskofu wa Congo siku ya Jumanne (26.08.2018) kutoa mwito wa kuchukuliwa hatua za haraka na kubwa kuwaokoa watoto wanaokabiliwa na baa la njaa wakati huu wa msimu wa kiangazi huko Kasai. Katika taarifa iliyotolewa na shirika la misaada la kanisa Katoliki, Caritas, Askofu Mkuu wa Congo, Marcel Madila, alionya kwamba iwapo watoto hawatasaidiwa, vifo vingi huenda vikatokea.

Mwandishi: Josephat Charo/afpe/dpae

Mhariri: Saumu Yusuf