1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Msumbiji wakomboa raia 87 katika mji wa Pemba

Saumu Mwasimba
24 Septemba 2021

Wanajeshi wa Msumbiji wamewaokoa  raia zaidi ya 80 kutoka jimbo la kaskazini mwa nchi hiyo, ambalo kwa ushirikiano na vikosi vya kigeni wameweza kulidhibiti tena kutoka mikononi mwa wapiganaji wa itikadi kali.

https://p.dw.com/p/40nN7
Mosambik Pemba | Militär
Picha: DW

Mataifa kadhaa ya Afrika yalipeleka wanajeshi wao nchini Msumbiji, kuisaidia nchi hiyo kuwatimua wapiganaji hao katika jimbo la Cabo Delgado lenye utajiri wa gesi, ambalo wamekuwa wakilishikilia tangu mwaka 2017.

Wapiganaji hao wenye mafungamano na kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiislamu, IS, walipata pigo kubwa mwezi Agosti, pale wanajeshi wa Msumbiji na Rwanda walipowafurusha kutoka makao yao makuu kwenye mji wa bandari wa Mocimboa da Praia.

Operesheni ya hivi karibuni ya kuwakomboa raia 87 katika mji mkuu wa jimbo la Cabo Delgado, Pemba, ilihusisha vikosi vya Rwanda na vya nchi wanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Kusini mwa Afrika, SADC.