1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wananchi Venezuela waunga mkono mabadiliko ya katiba

Aboubakary Jumaa Liongo16 Februari 2009

Rais Hugo Chavez wa Venezuela ameshinda katika kura za mabadiliko ya katiba na kuondoa kipengee katika katiba ya nchi hiyo kinachoweka ukomo wa kuwa rais.

https://p.dw.com/p/Guvq
Rais Hugo ChavezPicha: DW


Kwa mujibu wa tume ya uchaguzi ya Venezuela, Katika kura hiyo iliyofanyika jana Rais Chavez amepata asilimia 54 ya kura na kumfanya kuendelea kuwania urais hata baada ya kumalizika kwa kipindi chake cha miaka kumi mwaka 2013.


Akihutubia maelfu ya wafuasi wake muda mfupi uliyopita mara baada ya matokeo hayo kutangazwa, Rais Chavez amesema kuwa matokeo hayo yamepanua wigo wa majaaliwa ya nchi hiyo.


Rais Chavez ambaye ni mfuasi mkubwa wa siasa za kiongozi wa zamani wa Cuba Fidel Castro, amesema kuwa Venezuela kamwe sasa haitorudi katika zama za zamani alizoziita za kudhalilishwa na kudharauliwa.

Ushindi huo ni pigo kubwa kwa upinzani uliyosambaratika ambao katika miaka ya hivi karibuni uliweza kupiga hatua kuvuta uungwaji mkono.

Chavez aliingia madarakani mwaka 1999 kwa ahadi ya kupambana na rushwa ambapo amekuwa akiungwa mkono na watu wa hali ya chini kutokana na kuboresha sekta ya huduma za afya, shule pamoja na misaada ya chakula.