1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanne wafunguliwa mashtaka ya ugaidi Ubelgiji

9 Aprili 2016

Serikali ya Ubelgiji Jumamosi (09.04.2016) imewafungulia mashtaka watuhumiwa wengine wanne kwa kujihusisha na vitendo vya kigaidi kuhusiana na miripuko ya kujitowa muhanga iliosababisha maafa mjini Brussels na Paris.

https://p.dw.com/p/1ISdq
Polisi ikimdhibiti mtuhumiwa wakati wa msako uliopelekea kutiwa nguvuni kwa Mohamed Abrini huko Anderlecht (08.04.2016)
Polisi ikimdhibiti mtuhumiwa wakati wa msako uliopelekea kutiwa nguvuni kwa Mohamed Abrini huko Anderlecht (08.04.2016)Picha: Reuters/S. Dana-Kamran

Watu hao wanne Mohamed Abrini,Osama K,Herve B. M. na Bilal E. M. waliokamatwa katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita wamefunguliwa mashtaka ya kujihusisha na kundi la kigaidi kuhusiana na miripuko ya tarehe 22 Machi katika uwanja wa ndege wa Ubelgiji na kituo cha reli cha chini ya ardhi iliyouwa watu 32 na kujeruhi wengine 270.

Mtuhumiwa wa mashambulizi ya Paris Mohamed Abrini amekiri kwamba alikuwa ndie mtu aliyevalia kofia akiwa ameandamana na washambulaiji wawili waliojiripuwa Ibrahim el- Bakrouni na Najim Laachraoui katika uwanja wa ndege wa Brussels.

Kwa mujibu wa taarifa ya ofisi ya mwendesha mashtaka alikiri kuwepo kwake eneo la jinai na kwamba alilitupa koti lake kwenye pipa la taka na baadae kuiuza kofia yake.

Mtuhumiwa huyo wa tatu anashukiwa alikimbia bila ya kuliripua bomu lake ambalo baadae lilipatikana likiwa limetelekezwa uwanja wa ndege.

Abrini alikuwa akisakwa sana

Abrini alikuwa ni mtu anayesakwa kwa udi na uvumba barani Ulaya tokea camera za upelelezi za CCTV kumuonyesha akiwa pamoja na mtuhumiwa wa mashambulizi ya Paris Salah Abdelsalam katika kituo cha mafuta siku mbili kabla ya mashambulizi hayo yaliyouwa watu 130 nchini Ufaransa.

Kamera za upelelezi zilivomnasa mtuhumiwa.
Kamera za upelelezi zilivomnasa mtuhumiwa.Picha: picture-alliance/dpa/Belga/E. Lalmand

Wakati Abrini alikamatwa hapo Ijumaa Abdelsalam alikamatwa wiki mbili zilizopita ikiwa ni siku nne kabla ya washambuliaji wa kundi la Dola la Kiislamu kushambulia uwanja wa ndege wa Brussels na kituo cha reli cha chini ya ardhi mjini Brussels.

Waendesha mashtaka Jumamosi pia wamemfungulia mashtaka Osman K ambaye ni raia wa Sweden.

Inaaminika Osman Krayem wa mji wa Malmo aliwahi kwenda kupigana nchini Syria.Inadaiwa kwamba Krayem ndie aliepeleka mikoba iliotumika katika miripuko ya Brussels na alionekana katika kituo cha reli cha Maalbreek kabla ya mshambuliaji wa kujitowa muhanga Khalid el- Bakaroui kujiripuwa.

Kuhusika na kundi la kigaidi

Wengine waliofunguwa mashtaka ni Herve B. M raia wa Rwanda na Bilal E.M.Watuhumiwa wengine wawili waliokamatwa tokea Ijumaa waliachiliwa baada ya kusailiwa ipasavyo.

Polisi ya Ubeljiji wakati wa operesheni zao mjini Brussels (09.04.2016)
Polisi ya Ubeljiji wakati wa operesheni zao mjini Brussels (09.04.2016)Picha: Reuters/Y. Herman

Kufunguliwa mashtaka kwa watuhumiwa hao kunakuja kufuatia kamata kamata ambayo imetowa mwanga juu ya uhusiano walio nao na kundi la kigaidi la Dola la Kiislamu linaloaminika kuhusika na mashambulizi ya Paris na Brussels.

Washambuliaji kadhaa inaaminika waliwahi kuwepo Syria kwa muda fulani na kundi hilo ambalo limeapa kuendeleza mashambulizi yao barani Ulaya.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/Reuters/dpa

Mhariri : Bruce Amani