1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanne wauawa, 25 wajeruhiwa kwa mabomu ya M23

7 Februari 2024

Watu wanne wameuawa na wengine 25 wamejeruhiwa katika mashambulizi mawili ya mabomu katika mji mdogo wa Sake ulio karibu na vilipo vikosi vya Kulinda Amani vya Umoja wa Mataifa nchini Kongo (MONUSCO).

https://p.dw.com/p/4c8i6
DR Kongo | M23
Mpiganaji wa kundi la waasi la M23 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya KongoPicha: Arlette Bashizi/REUTERS

Mwandishi wa DW kwenye eneo hilo anasema wakaazi wa mji mdogo wa Sake wamekasirishwa sana na wanalaani tuhuma za ufisadi miongoni mwa maafisa wa jeshi wa la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC).

"Siye tulishachoka na vita vya Kongo. Tulishateseka, vita vya kila siku bila kuisha. Ni vita gani hivi? Miaka na miaka vita vya Batutsi." Alisema mmoja wa wakaazi hao, akimaanisha vita vya kundi la waasi wa M23, ambao Kinshasa inadai wanasaidiwa na nchi jirani ya Rwanda, madai yanayokanushwa na Kigali.

Soma zaidi: Jeshi la DRC lapambana na M23 Kivu Kaskazini

Pia wanamkosowa kamanda mpya wa Mkoa wa Kijeshi wa 34, Shora Mabondani, aliyewasili Goma wiki iliyopita, kwa kutokuchukuwa hatua madhubuti.

Kambi ya wakimbizi wa ndani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kambi ya wakimbizi wa ndani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Picha: Alexis Huguet/AFP

"Ba FARDC banakula rushwa sana. Bako na retirer ba militaires ku ligne de frond bana katala bapigane. Tuko na hasira sana kuona tuache mashamba, na manyumba. Ningelikuwa mkubwa, singeitika major ama colonel aende mu vita. Au moins batiye guerre kuba officier subalterne." Alisema mmoja wa wakaazi hao akitumia lahaja ya mashariki mwa Kongo inayochanganya Kiswahili na Kifaransa.

Hali ya dharura mjini Goma

Mji wa Goma, ambako wakaazi wa Sake wamekimbilia, unakabiliwa na mgogoro wa kibinadamu na hali ya dharura ya usalama.

Mapigano kati ya jeshi na waasi yanakaribia kuwa hatari, umbali wa kilomita saba tu kutoka Saké.

Kulingana na msimamo wa sasa wa waasi, mji wa Sake ndio eneo la mwisho kabla ya kufikia mji wa Goma.

Wakazi wa mji huu mdogo wamejikuta wakiwa wamekwama katikati ya miripuko ya silaha nzito na nyepesi, ikifanya maisha yao yawe magumu.

Kambi ya wakimbizi wa ndani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kambi ya wakimbizi wa ndani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Picha: Alexis Huguet/AFP

Soma zaidi: Mapigano kati ya kundi la M23 na Wazalendo yazua hofu Kongo

Mwakilishi mmoja wa shirika la kiraia ameiambia DW kwamba asilimia 70 ya wakaazi wa mji huo wa Sake wanaripotiwa kukimbilia mjini Goma, kulingana na shirika moja la kiraia.

"Huku watu wengi wameshakimbia maana vita vimekaribia Sake, na kitu chengine kilichowafanya watu watu wakimbie ni mabomu ambayo yameanguka mjini Sake na Masasi." Alisema mwakilishi huyo.

Wakati maelfu ya wakimbizi wanajazana kuelekea mji wa Goma, hofu inazidi kuongezeka na hali ya kibinadamu inazidi kuwa mbaya.

Imetayarishwa na Ruth Alonga/DW Goma