1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanne wauwawa wakati maelfu wakiandamana mpakani Gaza

Sekione Kitojo
31 Machi 2019

Maroketi matano yalirushwa kutoka Ukanda wa Gaza kwenda Israel,na kusababisha vifaru vya Israel kujibu kwa kushambulia maeneo ya  ya kundi la Hamas mapema  Jumapili,(31.03.2019) katika ya maandamano ya Wapalestina Gaza.

https://p.dw.com/p/3FxaS
Gaza | Plästinenser protestieren im Gaza-Streifen
Picha: Getty Images/AFP/M. Hams

Shambulio  hilo  la  maroketi  na  jibu  la  Israel  havikusababisha madhara yoyote, kwa  mujibu wa  jeshi  la  Israel  na  watu mashuhuda katika eneo  la  Gaza.

Gaza | Plästinenser protestieren im Gaza-Streifen
Vijana wa Kipalestina wakikimbia mabomu ya kutoa machozi ya jeshi la Israel katika mpaka wa Gaza na IsraelPicha: Getty Images/AFP/M. Hams

Vifaru vya  jeshi  la  Israel  vilishambulia  maeneo  ya  Hamas katikati ya  ukanda  wa  Gaza  na  mashariki  mwa  mji  wa  Gaza, mashuhuda wamesema.

Mamia  kwa  maelfu ya  wakaazi  wa  Gaza  walijikusanya  hapo mapema  katika  mpaka  na  Israel  kukumbuka  mwaka  mmoja tangu  maandamano  na  makabiliano  kuzuka  katika  eneo  hilo, lakini  hofu  ya  mauaji  makubwa  yaliepukwa  baada  ya  majadiliano yaliyoongozwa  na  Misri hapo  kabla.

Wapalestina wanne waliuwawa  na risasi  kutoka  jeshi  la  Israel , mmoja  wakati  wa  maandamano  kabla  ya  mkutano  mkuu  na wengine  watatu vijana  wa  umri  wa  miaka  17  katika  makabiliano jioni  ya  Jumamosi, wizara  ya  afya  katika  mji  wa  Gaza imesema. Wakaazi  wengine 316  wa  Gaza  walijeruhiwa.

Gaza | Plästinenser protestieren im Gaza-Streifen
Mamia ya waandamanaji wa Kipalestina katika uzio wa mpaka kati ya Gaza na IsraelPicha: Getty Images/AFP/M. Hams

Lakini  hofu  ya  kurejewa  kwa  maandamano  kama  hayo  na makabiliano  kwa  wale  walioshuhudia  zaidi  ya  Wapalestina 60 waliuwawa  hapo  Mei 14, wakati  Marekani  ilipohamisha  ubalozi wake  nchini  Israel  kwenda  Jerusalem, hayakutokea.

Israel  iliweka  maelfu  kadhaa  ya  wanajeshi  katika  mpaka, wakati kumbukumbu  hiyo  ikija katika  wakati nyeti  kabla  ya  uchaguzi  wa hapo  Aprili 9.

Upatanishi wa Misri

Misri  imejaribu  kufanya  upatanishi  kati  ya  Israel na  watawala wa  eneo  la  Gaza  kundi  la  mrengo  wa  Kiislamu  la  Hamas kuzuwia  ghasia.

Maafisa  wa  Hamas  wanasema  makubaliano  yamefikiwa  ambayo yatashuhudia  Israel  ikilegeza mzingiro  wake  unaoathiri  eneo  la Gaza , kwa  kupata  hali  ya  utulivu  wa  maandamano

Mamia  kwa  maelfu  ya  walijikusanya  katika  maeneo  matano katika  mpaka  huo  lakini  wengi  wa  watu  walibakia  mbali  na  uzio wa  mpaka.

Gaza Palästina Israel Protest
Kijana wa Kipalestina akiwa na ujumbe kwa Israel kuondoa mzingiro wa muongo mmoja sasa katika eneo hiloPicha: Reuters/M. Salem

Mashariki  mwa  mji wa  Gaza, makundi  madogo  ya  vijana wanaume walikaribia  uzio  na  kutaka  kuuvunja  mara  kadhaa  lakini walilazimishwa  kurejea  nyuma  na  mabomu ya  kutoa  machozi  ya vikosi  vya  Israel.

Waandamanaji  walirusha  mawe dhidi  ya  wanajeshi  wa  Israel.

Ujumbe wa  usalama  kutoka  Misri  ulifanya  ziara  katika  maeneo ya  maandamano  katika  mji  wa  Gaza, kama  walivyofanya viongozi  wa  Hamas Ismail Haniya  na  Yahya Sinwar.

Jeshi  la  Israel  lilisema  karibu "wafanya  ghasia  na waandamanaji" 40,000 walikusanyika  katika  maeneo mbali  mbali katika  mpaka  huo.

Jeshi  hilo  lilisema  maguruneti  na  viripuzi vilirushwa  dhidi  ya wanajeshi  hao, ambao  nao  walijibu "kwa mujibu wa  viwango vya utaratibu  wao  wa  kufanya  kazi".

Gaza Israel Palästina Konflikt
Vijana wa Kilaestina wakirusha viripuzi kutoka upande wa GazaPicha: Reuters/M. Torokman

Waandamanji  walikuwa  wakikumbuka  mwaka  mmoja  wa  wiki  ya maandamano  ya  ghasia  ya  kila  mara  ambamo  kiasi  ya Wapalestina 200  na  mwanajeshi  mmoja  wa  Israel waliuwawa.

Takriban  watoto  50  wa  Kipalestina  waliuwawa  katika  ukanda wa  gaza  tangu  maandamano  hayo  kuanza, kundi  la  hisani  la Save The Children  limesema.