1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapalestina waandamana kwa amani kuipinga Israel

Nyanza, Halima 25 Februari 2008

Israel yaonya kuwachukulia hatua kali wapalestina watakaoandamana hadi nchini humo

https://p.dw.com/p/DD4o
Wanafunzi wa kipalestina wajiunga katika maandamano GazaPicha: AP
Maelfu ya Wapalestina wameandamana kwa amani leo, ukanda wa Gaza kupinga vizuizi vilivyowekwa na Israel, hali ambayo imeleta ugumu zaidi wa maisha katika eneo hilo linalodhibitiwa na Hamas. Miongoni mwa walioandamana walikuwa ni watoto wa shule ambao kwa pamoja na watu wazima waliunda mfano wa mnyororo mrefu wa binadamu. Jeshi la Israel liliwekwa katika hali ya tahadhari, huku likitishia kushambulia waandamanaji hao iwapo wangejaribu kutumika nguvu kukatisha mpaka na kuingia katika ardhi yao. Waratibu wa maandamano hayo walikadiria watu elfu 40 hadi 50 kushiriki, lakini hata hivyo hali mbaya ya hewa iliathiri uwingi wa washiriki wa maandamano hayo. Maelfu ya watoto wa shule hao wakiungwa mkono na watu wazima, waliandamana kwa amani katika barabara ya Salahedin huku wakiwa wamebeba mabango yenye kulaumu Israel kwa kuzingira Gaza na kutaka Gaza ikolewe na matatizo hayo. Miongoni mwa walioandaa maandamano hayo kupinga hatua hiyo ya Israel kuzingira Gaza, Jamal Al Khudari alifafanua kuwa maandamano hayo ni ya amani ambayo watu wanaelezea kukataa kwao adhabu hiyo waliyopewa na Israel. Naye msemaji wa Hamas Fawzi Barhum amesema ujumbe wa maandamano hayo umeelekezwa kwa Israel na jumuia ya kimataifa na kuongeza kuwa anamatumaini hatua hiyo itasaidia. Wapalestina na mashirika ya kimataifa wamesema kuwa vikwazo hivyo vilivyowekwa na Israel dhidi ya Gaza vimekuwa ni adhabu kwa raia wa kawaida, hali inayosababisha uhaba wa chakula na kuletesha matatizo mengine kadhaa ya kibinadamu. Awali taarifa iliyotolewa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Israel, Tzipi Livni na Waziri wa Ulinzi Ehud Barak ilisema haitaingilia maandamano hayo ndani ya ukanda wa Gaza, lakini itahakikisha inalinda eneo lake na pia uvunjaji wowote wa sheria katika mpaka wake. Taarifa hiyo pia iliishutumu Hamas kwa kuwapanga raia katika juhudi hizo. Naibu Waziri wa Ulinzi wa Israel Matan Vilnai amesema watahakikisha hali haitorejea kama yaliyotokea kipindi cha nyuma. Aliendelea kusema, ''Tutafanya yaleyale tuliyoyafanya katika wimbi la mwanzo la Intifadha.. watu walipoanza kuandamana. Nimeshuhudia zaidi ya mara moja na tutachukua hatua muafaka. Hatutasita kutumia njia zinazohitajika kuzuia wasiingie katika ardhi ya Israel.'' Mwezi uliopita wapiganaji wa Kipalestina walibomoa ukuta wa mpaka unaotenganisha Gaza na Misri na kusababisha maelfu ya wakazi wa Gaza kuingia nchini Misri kununua chakula na mahitaji mengine kutokana na eneo lao kuwekewa vizuizi na Israel. Hata hivyo mpaka huo ulikuja kufungwa baadaye. Wakati huo huo kijana mmoja wa Israel amejeruhiwa baada ya roketi lililorushwa kutokea Gaza kupiga eneo la nyumba katika mji wa kusini wa Sderot.