1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapiganaji wafanya mashambulio Pakistan na Afghanistan.

Halima Nyanza6 Oktoba 2010

Watu wenye silaha wanaohisiwa kuwa ni kutoka katika kundi la Taliban leo wamechoma moto malori ya kubebea mafuta ya jeshi la Kujihami la NATO nchini Pakistan.

https://p.dw.com/p/PWWi
Kikosi cha kuzima moto nchini Pakistan, kikijaribu kuzima malori ya mafuta, baada ya wapiganaji kushambulia eneo hilo.Picha: AP

Hii ni mara ya nne kwa wiki hii kwa kundi hilo la kiislamu lenye msimamo mkali kwa madai ya kulipiza mashambulio yaliyosababisha mauaji yaliyofanywa na majeshi ya Marekani.

Afisa wa polisi katika mji ulioko kusini magharibi mwa Pakistan, wa Quetta Hamid Shakeel amesema wapiganaji walishambulia ghala lililokuwa limehifadhi malori 40, nje ya mji huo na kumuua mfanyakazi mmoja pamoja na kuteketeza  magari yapatayo 10.

Wapiganaji wa Taliban wamedai kuhusika katika shambulio hilo na mengine yaliyotokea wiki hii, ambapo takriban malori 60 yalichomwa moto na watu watatu kuuawa.

Kundi hilo limeapa kufanya mashambulio zaidi, ili kuvuruga  njia za usambazaji za NATO, kupitia Pakistan pamoja na kulipiza kisasi, mashambulio yanayofanywa  na Marekani ambayo yanawalenga wapiganaji wa Taliban na al Qaeda wakihusisha na madai ya mipango ya kufanya mashambulio ya kigaidi dhidi ya miji kadhaa barani Ulaya.

Akithibitisha hilo, balozi wa Pakistan nchini Uingereza Hussein Haqqan, amesema kuongezeka kwa mashambulio kaskazini mwa Wazirstan , kumekuja baada ya mashirika ya kijasusi kufumbua mpango wa mashambulio yanayolenga bara la Ulaya.

Aidha ameongezea kuwa shambulio la anga lililofanywa siku ya Jumatatu ya wiki hii nchini humo na kusababisha vifo vya wapiganaji wanane, wakiwemo Wajerumani watano, linahusiana pia na mipango hiyo.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere alipotakiwa kuthibitisha juu ya raia hao wa Ujerumani, alisema hawezi kuthibitisha hilo.

Aidha akizungumzia kitisho cha nchi yake kuwa miongoni mwa mataifa yanayolenga kushambuliwa kigaidi, amesema haoni dalili zozote za mashambulio nchini mwake.

Imeelezwa kuwa mipango ya mashambulio yaliyoripotiwa ambayo yalipangwa kufanywa katika nchi za Ujerumani, Ufaransa na Uingereza yalikuwa katika hatua za awali wakati mashirika ya kijasusi yalipoigundua.

Katika tukio jingine, raia wanane na polisi mmoja wameuawa na wengine 25 wamejeruhiwa baada ya wapiganaji kuuvamia na kuushambulia mssafara wa polisi katika mji wa kusini wa Afghanistan wa Kandahar.

Msemaji wa Gavana wa jimbo hilo Zalmay Ayubi amesema wapiganaji hao waliwashambulia polisi waliokuwa katika doria nje ya mji wa kandahar, na kusababisha milipuko kadhaa.

Nao maafisa wa hospitali wamesema wengi ya watu waliojeruhiwa katika tukio hilo ni wanawake na watoto, ambao wengi walijeruhiwa katika mlipuko wa pili, kutokana na watu katika eneo hilo kukusanyika baada ya kutokea mlipuko wa kwanza.

Wakati wapiganaji wakiendelea na mapambano yao, gazeti la Washngiton post limeripoti kuwa mazungumzo ya siri kati ya wawakilishi wa Taliban na serikali ya Rais Hamid Karzai yameanza kujadili hatua za kumaliza vita nchini Afghanistan.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mazungumzo bado yako katika hatua za mwanzo na kwamba ni ya kwanza kufanyika huku yakiwa yamepata idhini kamili kutoka kwa kiongozi wa Taliban Mohammad Omar, ambaye aliondolewa madarakani wakati Marekani ilipoivamia Afghanistan mwaka 2001, pamoja na kutoka kwa kundi la Wataliban wa Afghan, lenye makaazi yake nchini Pakistan la Quetta Shura.

Chanzo cha habari kilicho karibu na mazungumzo hayo kimesema kwamba pande zote mbili ziko makini kuweza kupata njia za kumaliza mapigano hayo.

Gazeti hilo limeelezea kuwa  wawakilishi wa kiongozi wa Taliban Mohammad Omar wamesisitiza wazi kwamba  majadiliano hayo hayatawezekana mpaka pale majeshi ya kigeni yatakapojiondoa nchini Afghanistan, lakini hata hivyo limesema kuwa kundi la Quetta Shura limeanza kujadili makubaliano ambayo yatajumuisha ushiriki wa baadhi ya wanachama wa Taliban katika serikali ya Afghanistan na pia kujadili makubaliano juu ya kujiondoa kwa majeshi ya Marejkani na ya Jumuia ya Kujihami ya NATO, katika muda uliokubaliwa.

Hata hivyo msemaji wa Rais Karzai Waheed Omer, akizungumza mjini Kabul alikataa kuthibitisha ama kukanusha taarifa hizo za kufanyika mikutano mipya.

Mazungumzo hayo yamewezeshwa, kutokana na mabadiliko ya sera ya utawala wa Rais Barack Obama, abapo hivi karibuni uliacha uamuzi wake wa kuyazuia mazungumzo kama hayo.

Mwandishi: Halima Nyanza(dpa, afp, Reuters)

Mhariri:Josephat Charo