1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapinzani wakuu wa rais Comoro wazuwiwa kugombea urais

Iddi Ssessanga
11 Februari 2019

Mahakama ya juu kabisaa nchini Comoro imewatangaza wagombea 13 watakaowania uchaguzi wa Rais mwezi Machi, na kuwazuwia wapinzani wakuu wa Rais Azali Assoumani.

https://p.dw.com/p/3D7Uz
Komoren Azali Assoumani Präsident
Rais wa Comoro Azali Assoumani. Picha: Getty Images/AFP/I. Youssouf

Wagombea 19 walijiandikisha kwa ajili ya uchaguzi wa Machi 24 na kati ya waliopitishwa, ni Asoumani tu anayeungwa mkono na chama cha siasa. Wengine wote wanashiriki kama wagombea binafsi. Azali aliyechaguliwa mwaka 2016, anatazamiwa kushinda uchaguzi huo.

Wapinzani wake wakuu walikuwa makamu wa zamani wa rais Mohamed Ali Soilih na Ibrahim Mohamed Soule, ambao juhudi zao za kuwania wadhifa huo zilitupiliwa mbali na mahakama ya juu ambayo imejazwa na washirika wa Azali pekee.

Mpango wa kupokezana madaraka miongoni mwa visiwa vitatu vya taifa hilo ulisaidia kuzuwia hali ya kutoridhika iliyotawala kwa miaka kadhaa pamoja na mapinduzi ya mara kwa mara mwishoni mwa miaka ya 1990.

Uchaguzi utafanyika chini ya vifungu vya katiba vilivyorekebishwa kwa utashi wa Azali katika kura ya maoni iliyobishaniwa Julai 2018. Mageuzi hayo yanamuwezesha rais kushika madaraka kwa mihula miwili ya miaka mitano kila mmoja badala ya muhula mmoja.

Iwapo Azali atashinda, atachukuliwa kuwa ndiyo anaanza muhula wake wa kwanza, jambo ambalo litamruhusu kuwania muhula wa pili mwaka 2024.

Karte Komoren EN
Ramani inayoonyesha visiwa vinavyounda Comoro.

Sababu za kuzuiwa wagombea

Soilihi alisema amezuiwa kugombea kwa sababu alituhumiwa kwa kuficha umiliki wa kampuni yenye thamani ya mabilioni ambayo hata hivyo amasema hajui lolote juu yake.

"Wagombea wote wa upinzani ambao wangetoa changamoto kwa Azali wamezuiwa," alisema, na kupinga kile alichokiita ucheleweshaji wa uchaguzi.

Soule alisema alizuiwa kwa sababu hati yake ilisainiwa na naibu katibu mkuu na siyo katibu mkuu Ahmed el-Barwane, ambaye alikuwa gerezani kwa miezi kadhaa kwa madai ya kumshambulia mwanajeshi. Upinzani umeparaganyika baada ya viongozi wake kadhaa kukamatwa.

Mahakama ya usalama imetoa hukumu kadhaa za vifungo vya gerezani kwa wanasiasa mashuhuri waliopinga kura ya maoni inayomruhusu Azali kurefusha muhula wake madarakani. Ikiwa duru ya pili itahitajika kwa kukosa mshindi wa moja kwa moja, itafanyika Aprili 21.

Katiba mpya imebakisha mzunguko wa urais miongoni mwa visiwa vitatu vya Grande Comore, Anjouane na Moheli, lakini kipindi kimeongezwa kutoka miaka mitano hadi kumi. Kisiwa cha Azali cha Grande Comore, hivi sasa ndiyo kinashikilia fursa hiyo.

Azali mwenyewe alianza kutwaa madaraka kwa njia ya mapinduzi dhidi ya kaimu rais wa nchi mwaka 1999 na alirudishwa madarakani hadi 2006 katika kura ya vyama vingi. Mwaka huo, madaraka yalibadilishwa kwa amani kwa mara ya kwanza tangu uhuru kutoka kwa Ufaransa mwaka 1975.

Hii leo, wakosoaji wa Azali wanachukulia kwamba amechukuwa mwelekeo wa kidikteta, akiwa na uwezekano wa kusalia madarakani hadi 2029.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe

Mhariri: Josephat Charo