1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waratibu wa maandamano Sudan kutangaza baraza la kiraia

Yusra Buwayhid
19 Aprili 2019

Wandalizi wa maandamano Sudan wamesema Ijumaa kwamba watatangaza baraza la mpito wanalotaka lichukue mamlaka kutoka kwa jeshi lililomuondoa madarakani rais Omar al-Bashir, baada ya miezi kadhaa ya maandamano ya kumpinga.

https://p.dw.com/p/3H5aQ
Sudan Proteste in Khartum
Picha: Getty Images/AFP/A. Mustafa

Tangazo hilo limetolewa huku maelfu ya wananchi wa Sudan wakiwa wanaandamana kuelekea makao makuu ya jeshi mji mkuu wa Khartoum, eneo ambalo ndiyo kitovu cha maandamano yaliyomuondoa al-Bashir madarakani baada ya kutawala kwa miaka 30 nchini humo. Yanatajwa kuwa ni maandamano makubwa kushuhudiwa tangu kuondolewa al-Bashir madarakani.

Waandamanaji wanalitaka jeshi- ambalo lilimtia nguvuni al-Bashir baada ya kumuondoa madarakani wiki iliyopita na kuanzisha baraza la mpito la kijeshi litakaloongoza kwa kipindi kisichozidi miaka miwili- liondoke madarakani na kuundwe serikali ya kiraia. Waandamanji hao wanasema wataendelea na maandamano hadi madai yao yatimizwe.

"Kama hatutobaki hapa itakuwa kama vile hatukufanya kitu, tutabaki hadi pale tutakapofanikiwa kuliondoa baraza la kijeshi," amesema mwanadamanaji Rania Ahmed mwenye umri wa miaka 26.

Muungano wa Wafanyakazi wa Sudan (SPA), ambao umekuwa mstari wa mbele kwa miezi minne kuandaa maandamano hayo, umesema utatangaza baraza la uongozi wa kiraia katika mkutano na waandishi habari hapo Jumapili.

Sudan Militärrat Abdel Fattah al Burhan
Jenerali Abdel Fattah al BurhanPicha: picture-alliance/AA

Waandamanaji hao wa Sudan wanahofia jeshi, ambalo lina wingi wa viongozi wa kijeshi walioteuliwa na al-Bashir, litang'ang'ania madaraka au litamteua mmoja wao kuingoza nchi.

Baraza la kijeshi kutokabidhi madaraka kwa raia

Baraza la kijeshi limesema liko tayari kutimiza baadhi ya madai ya waandamanaji, ikiwa ni pamoja  na kupambana na rushwa, lakini limeashiria kwamba haliko tayari kukabidhi madaraka kwa viongozi wa maandamano hayo. Limeongeza kwamba kipindi cha mpito cha miaka miwili kitafuatiwa na uchaguzi na kwamba jeshi hilo liko tayari kufanya kazi pamoja na baadhi ya wanaharakati wanaompinga al-Bashir pamoja na makundi ya upinzani na kuunda serikali ya mpito ya kiraia.

Al-Bashir ambaye uongozi wake ulikuwa umetawaliwa na migogoro, vita vya wenyewe kwa wenyewe pamoja na ufisadi, pia anasakwa na Mhakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC kwa mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya ubinadamu alioufanya katika jimbo la magharibi la Darfur.

Kwa sasa al-Bashir ameshikiliwa katika gereza la mjini Khartoum la Kober, lenye sifa mbaya ya kuwashikilia wafungwa wa kisiasa wakati wa utawala wake. Kaka zake kiongozi huyo alieondoshwa madarakani pamoja na washirika wake kadhaa wa karibu na viongozi wengine wa serikali iliyopita pia wamewekwa kizuizini katika gereza hilo.

Viongozi wa zamani wafunguliwe mashtaka

Madai ya waandamanaji hao pia yanajumuisha kufunguliwa mashtaka kwa viongozi wa zamani wa ngazi za juu wa iliyokuwa serikali ya al-Bashir kwa kuhusika na ufisadi pamoja na ukiukaji wa haki za binadamu, pamoja na kuvunjwa kwa vikosi vya kijeshi vya al-Bashir vilivyokuwa vikikandamiza upinzani na uasi nchini humo.

Sudan Unruhen Proteste in Khartum Kober Gefängnis
Gereza la Kober mjini KhartoumPicha: Getty Images/AFP

Mataifa ya Afrika na Mashariki ya Kati yamekuwa yakifuatilia kwa karibu hali inavyoendelea nchini Sudan. Uganda imesema wiki hii kwamba inaweza kumpa hifadhi al-Bashir iwapo itahitaji msaada huo, na Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini amependekeza kuwa mpatanishi wa mgogoro huo wa Sudan.

Jeshi la Sudan pia linajaribu kujiepusha kutumbukia katika mgogoro kati ya Qatar na mataifa ya Kiarabu yanayoongozwa na Saudi Arabia. Shirika la habari la serikali la SUNA limesema Alhamisi kuwa mkuu wa baraza la kijeshi la mpito, Jenerali. Abdel-Fattah Burhan, amemfuta kazi naibu waziri wa mambo ya nje Badr Eddin Mohammed kwa kutoa taarifa kwamba jeshi limekataa kukutana na wajumbe wa Qatar. Burhan pia amewafuta kazi manaibu waziri wa mawasiliano na maji, limeripoti shirika la habari la SUNA lakini bila ya kutoa sababu za kufutwa kazi kwao.

Wananchi wa Sudan wameshuhudia mfumuko wa bei, uhaba wa fedha na wa bidhaa za msingi. Wachambuzi wengi wanasema matatizo ya kiuchumi ya nchi yanatokana na matumizi mabaya ya fedha, rushwa na vikwazo vya Marekani dhidi ya Sudan pamoja na kupoteza mapato ya mafuta wakati eneo la kusini lilipojitenga na kuundwa taifa la Sudan Kusini mwaka 2011.