1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Warohingya waandamana Bangladesh

Sudi Mnette
15 Novemba 2018

Kiasi ya wakimbizi 1,000 wa jamii ya Rohingya wamefanya maandamano nchini Bangladesh kupinga hatua ya kuwarejesha nchini Myanmar kuepuka ukandamizaji wa jeshi la nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/38HcL
Bangladesch - Rohingya Zurückführung
Picha: picture-alliance/AP Photo/D. Yasin

Katika kambi ya Unchiprang, moja miongoni mwa makazi ya wakimbizi, karibu na wilaya ya Cox Bazar, afisa wa  anaehudumia wakimbizi nchini Bangladesh amekuwa akitangaza kwa kipasa sauti akiwataka Warohingya warejee katika taifa lao.

Taarifa hiyo ilisema imeandaa kila kitu kwa ajili ya safari yao ikiwemo mabasi sita, malori, vyakula. Na kusema imeweka kila mazingira wayatakayo ili mradi waondoke nchini Bangladesh. Inawaeleza kama watakubaliana na jambo hilo watapelekwa hadi mpakani katika kambi ya muda ya maandalizi ya safari. Lakini baadhi ya wakimbizi wanapingana na hatua hiyo "Kama tutapata haki zetu, tutakuwa na furaha kurejea, tunaweza kuondoka hata sasa. Lakini walitutesa sana, katika kiwango ambacho sina maneno ya kukielezea." alitambuliwa kwa jina moja la Shakina na mwezinwe Nurul Amin alisema "Tunaishi kambini kwa miezi 14, na sasa majina yetu yapo katika orodha ya kurejeshwa Burma, kwa hivyo tumetoka kambini kwa hofu ya kurejeshwa na kujificha hapa."

Serikali inalengo la kuwaondoa Warohingya

Bangladesch - Rohingya Zurückführung
Kambi ya Warohingya BangladeshPicha: picture-alliance/AP Photo/D. Yasin

Awali katika taarifa yake serikali  ya Bangladesh imeeleza kwamba mpango wa kuwarejesha nyumbani kwao takribani wakimbizi laki saba wa Kirohingya inapaswa kuanza leo, lakini kama watu hao watakuwa tayari kufanya hivyo. Hatua hiyo ilitangazwa pamoja na miito ya maafisa wa Umoja wa Mataifa na makundi ya haki za binaadamu kutaka zoezi hilo lisitishwe.

Hata hivyo Kamishna wa wakimbizi wa Bangladesh, Abul Kalam amegoma kusema lolote kwamba taifa lake litachukua uamuzi gani endapo wakimbizi hao watakataa kuondoka. Kwa mujibu wa makubaliano yaliosimamiwa na Umoja wa Mataifa kati ya Bangladesh na Myanmar, jamii hiyo ya wachache haiwezi kuondoshwa kwa lazima nchini Bangladesh. Hata hivyo makundi ya haki za binaadamu yanasema jumla ya watu 150 kutoka katika takribani familia 30 wameshafikishwa katika kambi ya muda mpakani kwa ajili ya kuwarejesha Myanmar.

Wimbi kubwa la wakimbizi wa Kirohingywa lilianza mwezi wa nane mwaka uliopita, baada ya vikosi vya usalama vya Myanmar kuanzisha operesheni ya ukandamizaji wa kikatili dhidi yao baada ya mapigano ya makundi yenye kujihami na silaha nchini humo. Kiwango hicho ukandamizaji jumuiya ya kimataifa ilikiita kuwa ni uangamizaji wa kikabila na mauwaji ya halaiki.

Idadi kubwa ya watu nchini Myanmar, wengi wao kutoka jamii ya Wabudha haiwakubali jamii ya wachache ya Waislamu wa Rohingya, wakiwatazama kama watu wanaoishi nchini humo kinyume na sheria wakitoka Bangladesh.

Mwandishi: Sudi Mnette APE
Mhariri: Iddi Ssessanga