1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasanii warejea kazini Pakhtunkhwa

Admin.WagnerD15 Januari 2014

Wasanii wa muziki na maigizo wameanza kufanya shughuli zao tena katika mkoa wa Pakhtunkhwa nchini Pakistan, kufuatia kuondolewa kwa kundi la Taliban katika maeneo mengi ya mkoa huo.

https://p.dw.com/p/1Ar3s
Picha: picture alliance / Yvan Travert / akg-images

Kwa muda mrefu wasanii wa muziki na maigizo katika jimbo la Khyber Pakhtunkhwa, kaskazini mwa Pakistan walipoteza sauti yao, baada ya wapiganaji wa Taliban kupiga marufuku muziki na maigizo walivyosema vinakwenda kinyume na mafundisho ya Uislamu. Lakini baada ya mabadiliko katika miezi michache iliyopita, muziki umerejea tena katika maeneo mengi ya jimbo hilo

Watu wa kabila la Pakhtun ambao ndio wenyeji wa jimbo hilo ni wapenzi wa muziki kwa asili yao. Lakini kati ya mwaka 2008 hadi 2013 wanamuziki walikabiliwa na wakati mgumu, wakati jimbo hilo likiwa chini ya utawala wa chama kinachowapinga watalibani cha Awami National Party (ANP), na wapiganaji walifanya mashambulizi ya miripuko ya mabomu na kujitoa mhanga. Wataliban waliwazuwia wanamuziki kuendesha shughuli zao.

Izzat Majeed, mwanzilishi wa studio ya kurekodi muziki ya Sachal.
Izzat Majeed, mwanzilishi wa studio ya kurekodi muziki ya Sachal.Picha: Sachal Studio

Lakini wakati ambapo ushwawishi wa kundi la Talibani unazidi kupungua katika jimbo hilo, na serikali mpya ya jimbo ikiwahamasisha wasanii tangu ilipoingia madarakni, muziki umeanza kurejea. Mwanamuziki Gul Pana, aliliambia shirika la habari la IPS kuwa wanamuzi wengi na wapiga vyombo wamereja kazini kutokana na kupungua kwa vitendo vya ugaidi.

Mauaji na vitisho dhidi ya wasanii

Wilaya ya Swati iliyoko katika mkoa huo wa Pakhtunkhwa, ilikuwa ikijulikana kutokana na wanamuziki wake na wacheza dansi. Eneo hilo la milima lina mandhari kadhaa za mito ambazo zilikuwa zinatumika katika utengenezaji wa filamu na nyimbo. Lakini eneo hilo lilishiwa wasanii kuanzia mwaka 2007 hadi 2010 kutokana na adhabu zilizokuwa zinatolewa kwao na Taliban.

Mwaka 2009 Watalibani walimuuwa mcheza muziki maarufu Shabana wilayani Swati, na kuwalaazimisha wengine kuachana na taaluma yao kwa kuhofia kulengwa na kundi hilo. Lakini hivi sasa muziki unaweza kusikika kutoka milima na mabonde ya Swati. Watalibani waliondolewa kutoka wilaya ya Swati kupitia operesheni ya kijeshi mwaka 2010.

Maonyesho ya muziki yamerejea pia mjini Peshawar, ambao ni mji mkuu wa mkoa wa Khyaber Pakhtunkhwa, baada ya chama cha Pakistan Tareek Insaf PTI, cha mchezaji wa zamani wa kriketi aliegeuka mwanasiasa Imran Khan, kuingia madarakani kikiongoza muungano katika jimbo hilo. Mpiga kinanda Shah Sawar, aliiambia IPS kuwa watu wanawaalika hivi sasa katika shughuli zao binafsi na kuwatunza pesa waigizaji kuonyesha furaha yao. Sawar mwenye umri wa miaka 25, anasema hivi karibuni alifanya onyesho mbele ya Imrani Khan na alitunzwa.

Kiongozi wa chama cha PTI Imran Khan.
Kiongozi wa chama cha PTI Imran Khan.Picha: Reuters

Ukumbi wa muziki wajaa tena

Ukumbi wa Nishtar, ambao ndiyo pekee mjini Peshawar, umeanza kufanya kazi kama kawaida na karibu unakuwa na maonyesho ya muziki karibu kila siku. Afisa wa ukumbi huo ambao unaendeshwa na serikali, Karam Khan, alisema kuwa wanapokea simu kila siku, na zaidi ya hapo, wasanii wa eneo hilo na waimbaji kutoka maeneo mbalimbali ya nchi wanafanya maonyesho yao ukumbini hapo.

Kila shughuli inayofanyika katika ukumbi huo unaokalisha watu 600 inavutia mashabiki ambao huanza kuingia ukumbini kabla ya maonyesho kuanza. Siku za ukumbi wa Nishar kuendelea kufungwa kutokana na vitisho vya Taliban zimepita, hali imerudi kawaida na shughuli za kitamaduni zimeshika kasi, alisema karam Khan.

Mrembo wa zamani Mashooq Sultan pia anafurahishwa na chama cha Imran Khan. Anasema amekuwa baraka kwa wasanii zaidi ya 10,000 ambao hawakuwa na ajira wakati chama hicho kilipoingia madarakani. Anasema ilikuwa vigumu kwake kuihudumia familia yake kwa sababu kulikuwa na shughuli ndogo sana za kimuziki, lakini kipindi cha miezi sita iliyopita kilikuwa kizuri sana kwao, na kuongeza kuwa wanamshukuru Khan kwa kurekebisha hali.

Eneo hilo lililoko mpakani mwa Pakistan na Afghanistan bado linaendelea kupambana na wapiganaji. Baadhi ya maeneo ya Khayber Pakhtunkwa ambako Watalibani bado wana ushawishi yanakabiliwa na vikwazo vya muziki mapaka leo, lakini Mashooq Sultan anasema muziki hauwezi kuzuwia na kwamba Wataliabana hawawezi kuupiga maruku milele.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/ips
Mhariri: Mohammed Khelef