1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasemavyo wahariri wa Ujerumani

Admin.WagnerD18 Februari 2014

Jumanne hii wahariri wanazungumzia kadhia ya mwanasiasa wa chama cha SPD Sebastian Edathy na mgogoro unaofukuta serikalini, sakata la Aksofu mkuu wa jimbo la Limburg na mgogoro wa wa kisiasa nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/1BAow
Koalitionsverhandlungen Symbolbild Schachfiguren
Picha: imago/Christian Ohde

Mhariri wa gazeti la Straubinger Tagblatt analimulika sakata la mwanasiasa wa chama cha Social Democratic-SPD, Sebastian Edathy kuhusiana na picha za ngono za watoto kwa kusema:

Bila shaka Merkel hajakubaliana na namna SPD kupitia matamshi ya kiongozi wake bungeni Thomas Opperman, ilivyovitendea vyama ndugu vya CDU/CSU, ambavyo ni mshirika katika serikali ya muungano na SPD, na sasa inajaribu kutoa machozi ya mamba. Ingawa mwenyekiti wa SPD Sigmar Gabriel alijaribu kulipunguza makali suala hilo, chama chake kitalipa gharama kutokana na hila hii. Hasa chama cha CSU kinapoongeza shinikizo, kiongozi wake Horst Seehofer atataka fidia ya kisiasa. Tayari kwa sababu anataka kulizuwia, hiyo inamuweka katika hatari zaidi kutokana na ukaribu wake na Peter-Hans Friedrich, waziri wa kilimo aliejiuzulu.

Mhariri wa gazeti la General-Anzeiger naye ameandika juu ya sakata hilo, akisema huenda likatumiwa na vyama vya muungano kuilaazimisha SPD kujadili upya masharti ya muungano, yakiwemo kustaafu kwa mapema, kima cha chini cha mshahara na kodi inayotozwa magari makubwa. Mhariri huyo anasema:

Kwa uchache tu, jambo linalojitokeza ni kufanya mazungumzo mapya, ambayo yatasahihisha matokeo yaliyokwenda kombo - na hii itakuwa kwa gharama ya SPD. Lakini hata ikiwa hilo litatokea, wiki za kuaminiana zimekwisha. Muungano huu hautakuwa tena na msingi ulikoasisiwa na vyama vya CDU/CSU na SPD wakati wa majira ya mapukutiko.

Mhariri wa gazeti la Saarbrücker anasema kama vyama vya muungano vingefahamu kuwa kadhia ya Edathy ni tatizo la SPD na si la CDU na CSU, lingekuwa jambo la uwerevu kwao kusubiri hadi mambo yatulie, hasa kwa kuzingatia kuwa hili sio suala la vyama, bali ni la kitaifa.

Lakini Mhariri wa gazeti la Südwest Presse, yeye ameandika kuhusiana na sakata la matumizi mabaya ya fedha linalomkabili Askofu mkuu wa jimbo la Limburg hapa Ujerumani. Mhariri huyo amesema:

Kama bado kuna mtu mwenye kumhurumia Askofu Franz-Peter Tebartz-van Elst, basi mtu huyo anapaswa kumshauri kwa kumuambia kuwa: Chukuwa kilemba chako na uondoke. Ni kujiondoa kwake kwa hiari tu, na kuonyesha busara, kunakoweza kuliepusha Kanisa Katoliki na madhara makubwa aliyolisababishia. Hata hivyo, kuondoka tu kwa Tebartz-van Elst, hakutatuwi tatizo lililojificha la Kanisa Katoliki, ambalo ni mfumo dume usiyo na udhibiti, na ambao unaruhusu matumizi mabaya ya fedha uliyogunduliwa kwanza na tume ya uchunguzi. Ni wakati wa kufanya mageuzi.

Mhariri wa gazeti la Badische Neueste Nachrichten amayemulika tena maandamano ya nchini Ukraine, kufuatia ziara ya viongozi wa maandamano hayo mjini Berlin. Mhariri huyo anasema:

Licha ya kuendelea kwa wiki kadhaa, upinzani umefanikiwa kupata tahfifu chache tu kutoka kwa serikali. Hilo linatokana pia na udhaifu wa viongozi wake. Mapinduzi ya Ulaya hayajabadilisha chochote kuhusiana na tatizo la msingi la Ukraine. Nchi hiyo bado inaendelea kudhibitiwa na makundi mbalimbali ya kikabila, kundi lenye nguvu zaidi ni la kabila la Donezk, lake rais Viktor Yanukovych. Familia yake imepata utajiri mkubwa katika kipindi cha miaka mitatu tu, na hii imedhihirika kwa Yanukovych ambaye amebanwa katika wiki zilizopita, kuridhia baadhi ya makubaliano kwa shingo upande.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga

Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman