1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASEMAYO WAHARIRI

Abdu Said Mtullya15 Desemba 2010

Pamoja na masuala mengine wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanamzungumzia Waziri Mkuu wa Italia,Silvio Berlusconi.

https://p.dw.com/p/QaZC
Waziri Mkuu wa Italia Silvio Berlusconi.Picha: AP

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya Waziri Mkuu wa Italia Silvio Berlusconi,juu ya mwanzilishi wa tovuti ya Wikileaks na kuhusu mgogoro unaoikabili sarafu ya Euro.

Juu ya Berlusconi mhariri wa gazeti la Schwäbische anasema lingekuwa jambo zuri laiti angeshindwa katika kura za kutokuwa na imani naye. Lingekuwa jambo la furaha kwa Italia iwapo Berlusconi angeliondoka kabisa kwenye ulingo wa kisiasa.Kwani mpaka sasa hajafanya chochote licha ya kushughulikia mambo yake ya kibinafsi. Mageuzi aliyoahidi kuyaleta hayajaonekana mpaka leo.Lakini mhariri wa gazeti la Flensburger Tageblatt anasema tatizo la Italia siyo Berlusconi, bali ni udhaifu wa upinzani. Mhariri huyo anaeleza kuwa jambo baya katika siasa za nchini Italia ni kwamba kwa sasa hakuna mtu mwenye uwezo wa kuitoa Italia kutoka kwenye shimo la uchafu.Msiba wa Italia ni udhaifu uliopo katika upinzani.

Na mhariri wa Berliner Zeitung anasema hata kama waziri Mkuu Berlusconi angelishindwa katika kura ya kutokuwa na imani naye, haina maana kwamba angeliondoka. Sababu ni kwamba Italia yote imefukizwa uturi unaotoka kwenye televisheni yake.

Mhariri wa gazeti la Handelsblatt anazungumzia juu ya mgogoro unaoikabili sarafu ya Euro.
Anasema ikiwa Benki Kuu ya Ulaya itaendelea kununua dhamana kwa bidii na baadae kuziuza, hatua hiyo inaweza kuiwezesha Benki hiyo kujenga mtaji unaohitajika. Lakini pia inawezekana ikapata hasara.Lakini muhimu ni kuchukua hatua ili kuutatua mgogoro unaoikabili sarafu ya Euro. Na kwa kadri hatua zinavyochukuliwa mapema ndivyo gharama zitakavyokuwa ndogo.

Gazeti la Nordwest linatoa maoni juu ya Julian Assange-mwanzilishi wa tovuti ya Wikileaks inayoendelea kuchapisha maalfu ya nyaraka za siri.Bwana Assange bado yumo jela nchini Uingereza akiwa anakabiliwa na tuhuma za ubakaji. Juu ya mtu huyo gazeti la Nordwest linasema litakuwa jambo la manufaa kwa wote, ikiwa tuhuma za ubakaji zinazomkabili Assange zitazingatiwa , mbali kabisa na shughuli za tovuti yake. Lakini bado pana swali, jee , Assange ni mpenda ubinadamu kama alivyokuwa Robin Hood au ni mtu wa hatari anaetaka vurumai.?

Mwandishi/MtullyaAbdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri /Abdul-Rahman