1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON : Uamuzi wa Korea Kaskazini wakaribishwa

1 Novemba 2006
https://p.dw.com/p/CCxB

Serikali duniani kote hapo jana zimepongeza taarifa kwamba Korea Kaskazini imekubali kuanza tena mazungumzo juu ya mpango wake wa nuklea na kutelekeza silaha za nuklea.

Rais George W. Bush wa Marekani amesema ameridhishwa sana na hatua iliofikiwa baada ya Korea Kaskazini kurudia ahadi yake ya kutokomeza silaha zake za nuklea ili iweze kupatiwa hakikisho la usalama na ridhaa nyenginezo.

Majirani wa Korea Kaskazini Japani na Korea Kusini zimekuwa nchi za kwanza kukaribisha uamuzi huo ambao umekuja wiki tatu tu baada ya Korea Kaskazini kufanya jaribio lake la kwanza la bomu la nuklea.Urusi ikikaribisha habari hizo imeonekana kutahadharisha juu ya uwezekano wa kufanyika kwa mazungumzo hayo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan pia ameungana na itikio hilo la kimataifa kupongeza uamuzi wa Korea Kaskazini.

Korea Kaskazini ilikuwa imesusia mazungumzo ya pande sita yenye kuzihusisha China,Japani,Korea Kusini,Urusi na Marekani tokea mwezi wa Novemba mwaka jana.