1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON : Wabunge wadai mabadiliko Iraq

14 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBiq

Wabunge waandamizi wa chama cha Republican wamemtaka Rais George W. Bush wa Marekani kuanza kurasimu mipango ya kuondowa wanajeshi kutoka Iraq.

Lakini mpango wa maseneta John Warner na Richard Lugar tafauti na madai ya wabunge wa chama cha Demokratik hauweki tarehe zenye kushinikiza kuondolewa kwa wanajeshi hao wa Marekani.Muswada wao utaitaka Ikulu ya Marekani kubuni mipango ambayo itaweza kutekelezwa kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Wametowa pendekezo lao hilo ikiwa ni siku moja baada ya Rais Bush kukataa mabadiliko yoyote yale kwa mkakati wake wa vita wa hivi sasa.

Bush akizungumza na washauri wake wakuu wa kijeshi mjini Baghdad na Washington kwa njia ya video amesisitiza juu ya makakati wake huo na ulazima wa kushinda vita vya Iraq.

Bush amesema kile kinachotokea Iraq kinaigusa Marekani kwamba Iraq ya umwagaji damu na machafuko itaathiri usalama wa Marekani na Iraq ambayo itaweza kujitawala yenyewe na kutowa huduma za msingi kwa wananchi wake na kuwa mshirika katika vita dhidi ya ugaidi itamaanisha kwamba wote wamekubali changamoto hiyo kubwa na kuweka msingi wa amani kwa ajili ya watoto wao na wajukuu.

Kwa upande wa maseneta wa chama chake mwenyewe Bush cha Republican Lugar ni mmojawapo wa wabunge wa chama hicho mwenye uzoefu mkubwa kabisa katika masuala ya kigeni na kijeshi na hivi karibuni amekuwa akizidi kushutumu vita vya Iraq na kujiunga na shinikizo la wabunge wa Demokratik wanaotaka kumalizika kwa mzozo wa vita hivyo vya Irak uliodumu kwa miaka minne sasa.