1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON.Majeshi ya Marekani yamepata msukosuko nchini Irak akiri Bush

26 Oktoba 2006
https://p.dw.com/p/CCzG

Rais Geroge .W. Bush wa Marekani amekiri kwamba majeshi yake yamepata msukosuko mkubwa nchini Irak lakini wakati huo huo ametetea sera za serikali yake juu ya vita ya Irak.

Jumla ya wanajeshi 91 wa Marekani wameuwawa nchini Irak katika mwezi huu wa Oktoba pekee.

Hatua hiyo imezusha miito inayoitaka Marekani kuyaondosha majeshi yake kutoka nchini humo.

Huku uchaguzi wa kati ukiwa umekaribia rais Bush alisema katika mahojiano na waandishi wa habari katika ikulu ya White House kwamba anasikitishwa na hali ya kuongezeka kwa vurugu nchini Irak.

Habari zaidi kutoka Irak zinasema kumezuka mapambano baina ya majeshi ya muungano nchini Irak na wanamgambo katika kitongoji cha Sadr mjini Baghdad.

Wizara ya mambo ya ndani ya Irak imetoa taarifa kwamba watu wanne wameuwawa na wengine 20 wamejeruhiwa.

Kitongoji cha Sadr ni ngome ya kiongozi wa kidini Moqtada al Sadr.