1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

G20 Gipfel Abschluss

Charo Josephat/ Karl Zawadzky3 Aprili 2009

Mkutano wa G20 mjini London umefaulu

https://p.dw.com/p/HPTN
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel (kushoto) na rais wa Ufaransa Nicolas SarkozyPicha: AP

Mkutano wa nchi zilizoendelea kiviwanda na zinaoinukia kiuchumi duniani za G20 uliomalizika jana mjini London Uingereza haukuyamaliza matatizo yote ya kiuchumi yaliyosababishwa na mgogoro wa kiuchumi duniani. Lakini hata hivyo umeweka msingi wa hatua muhimu zitakazochukuliwa kufanya mageuzi katika mifumo ya fedha ya kimataifa ili kuzuia mgogoro mwingine wa kiuchumi kutokea.

Matokeo ya viongozi wa serikali na nchi za G20 mjini London ni hatua muhimu kuimarisha masoko ya fedha ya kimataifa na yanaimarisha matumaini ya kufikia mwisho wa mporomoko wa uchumi. Kuna sababu mbili kwa nini mkutano wa London umefaulu: Kwanza viongozi wa kundi la nchi 20 hawakuruhusu tofauti zao ziwafanya kupoteza nafasi muhimu ya kutafuta ufumbuzi kwa tatizo la uchumi.

Kwa upande mwingine kansela wa Ujerumani Angela Merkel na rais wa Ufaransa Nicholas Sarkozy kwa ukakamavu wao wamefaulu kuwashawishi viongozi wengine wa nchi za G20 kuanzisha sheria imara kusimamia mifumo ya fedha. Huu lakini haukuwa ushindi kwao peke yao kwani hata rais wa Marakani Barack Obama alitaka kuundwe sheria mpya.

Wazo la rais Obama la kutaka fedha zaidi zitolewe na serikali ili kufufua uchumi halikuungwa mkono kwenye mkutano wa London. Marekani imetambua changamoto zinazoyakabili mataifa ya Ulaya.

Wajumbe wa mkutano wa London walizingatia kwa makini kukabiliana na athari za mgogoro wa kiuchumi. Wamejadili hatua za serikali kuzembea sekta ya fedha kwani sheria hafifu zilizotumika ziliruhusu makosa mengi kutokea ambayo yameutumbukiza ulimwengu mzima katika mgogoro mkubwa wa kiuchumi.

Wanaobeba dhamana ni wafanyakazi wa mabenki wa mjini New York Marekani na mjini London Uingereza. Miji hii ndio chimbuko la mgogoro wa kiuchumi unaoikabili dunia. Matokeo yake ni kwamba katika siku za usoni masoko ya fedha na washikadau wote watachunguzwa kwa makini kuhakikisha mgogoro mwingine wa kiuchumi hautokei tena.

Ishara ya mkutano wa London iko wazi kabisa: Kutafanyika mageuzi makubwa katika mifumo ya fedha ya kimataifa kwa lengo la kutambua na kuyazuia makosa na kudhibiti kufilisika kwa mabenki makubwa na taasisi nyengine za fedha. Kwa hili viongozi wanatakiwa kushirikiana kwa karibu na Fuko la Fedha la Kimatafia, IMF, kutambua hatari zinazoyakabili masoko ya fedha na kupendekeza hatua za kuzuia mgorogoro wa kiuchumi kutokea.

Katika kipindi kifupi fedha za shirika la IMF zitaongezwa marudufu na baadaye kuongezwa mara tatu ili kuweza kuzisaidia na mikopo nchi wanachama zinazobiliwa na changamoto kutokana na mgogoro wa kiuchumi. Nchi zinazotumiwa kama pepo na watu na mashirika yanayopenda kukwepa kulipa kodi, zitafuatiliwa kwa karibu.

Mkakati wa kansela Merkel na rais Sarkozy bado uko wazi. Licha ya kiwango cha kutisha cha mgogoro wa kiuchumi, kulikuwa na nafasi rahisi ya kukubaliana juu ya hatua zitakazozuia makosa kutokea kwenye masoko ya fedha. Iwapo kutatolewa tena fedha za kuufufua uchumi, basi hatua hiyo itahujumu ari ya kufanya mageuzi.

La kuchunguzwa kwa karibu ni hatua ya kansela Merkel na rais Nicholas Sarkozy kukataa kusitolewe fedha zaidi kuufufua uchumi. Hatua zilizochukuliwa hivi sasa kukabiliana na mgogoro wa kiuchumi kwa mujibu wa Fuko la Fedha la Kimataifa zitaufanya uchumi ukue kwa asilimia mbili kufikia mwisho wa mwaka ujao.

Kwa hiyo ni sawa kabisa kuanza kutafakari kuhusu wakati baada ya kumalizika mgogoro wa kiuchumi hususan ikizingatiwa mzigo mkubwa wa deni litakalotokea. Bila shaka changamoto nyengine kubwa itakuwa ni kukabiliana na mgogoro wa kiuchumi na kuzuia mgogoro mwingine kutokea.