1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasiwasi juu ya hatima ya mateka Algeria

19 Januari 2013

Hali ya sintofahamu imetanda juu ya majaliwa ya raia wa kigeni waliotekwa nyara kwenye mtambo wa gesi nchini Algeria, ambako watekaji wao wanataka mbadilishano wa wafungwa na mwisho wa operesheni za Ufaransa nchini Mali.

https://p.dw.com/p/17NJ2
Mtambo wa gesi wa In Amenas nchini Algeria
Mtambo wa gesi wa In Amenas nchini AlgeriaPicha: Reuters

Wapiganaji wenye mafungamano na mtandao wa al-Qaida wamekaririwa na shirika la habari la Mauritania, ANA, wakisema bado wanawashikilia raia saba wa kigeni, sehemu mmoja ndani ya jangwa la Sahara karibu na mpaka baina ya Algeria na Libya. Mateka mmoja raia wa Marekani, ambaye ametambulishwa kama Frederick Buttacio, amethibitishwa kuuawa. Afisa wa usalama wa Algeria amesema idadi ya mateka hao inafika watu 10.

Kipaumbele kwa maisha ya mateka

Waziri wa nishati wa Algeria Youcef Yousfi akiwatembelea hospitalini mateka waliokombolewa
Waziri wa nishati wa Algeria Youcef Yousfi akiwatembelea hospitalini mateka waliokombolewaPicha: picture alliance / dpa

Akizungumza mjini Washington, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani Hillary Clinton amesema hali hiyo ni ''ngumu na ya hatari kubwa''. Bi Clinton ambaye alikuwa akiambatana na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Japan, Fumio Kishida, ameitaka Algeria kulipa kipa umbele suala la usalama wa mateka.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Laurent Fabius amethibitisha kifo cha mateka mmoja wa kifaransa. Maafisa wa Marekani wamesema ndege ya jeshi la nchi hiyo imeanza kuwasafirisha mateka walioachiwa, bila kutoa taarifa zaidi kuhusu idadi ya mateka wa kimarekani.

Mbadilishano wa wafungwa

Msemaji wa wapiganaji wa kiislamu ambaye yuko karibu na kiongozi wao Mokhtar Belmokhtar, ameliambia shirika la habari la Mauritania, ANA, kwamba kundi lao linalojiita ''saini ya damu'' bado linao mateka 3 raia wa Ubelgiji, wamarekani 2, mjapani mmoja, na muwingereza mmoja. Ubelgiji hata hivyo imesema haiamini kama kuna raia wake aliyekamatwa.

Mpiganaji nguli wa kiislamu Mokhtar Belmokhtar anayeongoza wateka nyara.
Mpiganaji nguli wa kiislamu Mokhtar Belmokhtar anayeongoza wateka nyara.Picha: picture alliance / dpa

Shirika la ANI lilisema kuwa mpiganaji mahiri wa kiislamu, Belmokhtar anataka wafungwa wawili wa kimarekani wabadilishwe na Sheikh kipofu raia wa Misri Omar Abdul Rahman na mpakistani Aafia Saddiqui, ambao wamefungwa nchini Marekani kwa hatia ya ugaidi. Hata hivyo, msemaji wa wizara ya nchi za nje ya Marekani Victoria Nuland amesema Marekani haijadiliani na magaidi.

Kuna idadi kubwa ya wafanyakazi wa mtambo wa gesi wa In Amenas ambao bado hawajulikani waliko, wakiwemo wajapani 10, na raia 8 wa Norway.

Algeria imekosolewa vikali kuhusu jinsi ilivyoushughulikia mzozo huo wa utekaji nyara kwa kuanzisha operesheni ya kijeshi kwa pupa. Duru za kiusalama zimearifu kuwa mateka 12 wamekufa, pamoja na watekaji nyara 18.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE

Mhariri: Stumai George