1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasiwasi waongezeka eneo la Ghuba

Lilian Mtono
19 Julai 2019

Hali ya wasiwasi katika eneo la Ghuba imezidi kuongezeka, baada ya rais Donald Trump wa Marekani kusema wameiharibu ndege isiyo na rubani ya Iran katika lango la bahari la Hormuz

https://p.dw.com/p/3MIwe
USS Boxer
Picha: Getty Images/U.S. Navy/MCSN Craig Z. Rodarte

Hata hivyo Iran inakana madai ya kudunguliwa kwa ndege yake. 

Shambulio hilo limekuwa la kwanza la kijeshi la Marekani dhidi yaIran kufuatia msururu wa kuongezeka kwa visa vibaya baina ya mataifa hayo. Rais Trump alitangaza hapo jana akiwa ikulu ya White House kwamba manowari yake ya USS Boxer ilichukua hatua hiyo aliyoiita ya kujilinda dhidi ya ndege hiyo isiyo na rubani ya Iran aliyosema ilikuwa ikitishia usalama wa manowari hiyo pamoja na wafanyakazi wake.

Trump alisema ndege hiyo ilidunguliwa mara moja baada ya kuisogelea manowari hiyo kwa umbali wa mita 914 na kupuuza wito wa wanajeshi wake kuitaka kutokaribia zaidi manowari hiyo. Trump alisema "ndege hiyo iliharibiwa mara moja.

Hii ni moja ya hatua za karibuni katika mlolongo wa visa vya uchokoti wa Iran dhidi ya operesheni zinazofanywa na manowari kwenye eneo la mpaka huru wa bahari. Marekani ina haki ya kulinda watumishi na mali zake, na ninayaomba mataifa yote kulaani jaribio hili la Iran la kuvuruga uhuru wa kuendesha shughuli na biashara ya kimataifa."

Iran |  Mohammad Javad Zarif
mwanadiplomasia wa juu wa Iran Mohammad Javad Zarif alisema hana taarifa ya kuangushwa kwa ndege ya IranPicha: YJC

Hata hivyo, waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohamad Javad Zarif jana aliwaambia waandishi wa habari kwamba hakuwa na taarifa yoyote ya kudunguliwa kwa ndege yake isiyo na rubani. Alisema wakati alipowasili makao makuu ya Umoja wa Mataifa, mjini New York kuhudhuria kikao na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres.

Lakini naibu waziri wake Abbas Araqchi mapema hii leo amekana taarifa hizo kwenye ukurasa wa twitter, akisema hakuna ndege ya Iran iliyopotea, na kuongeza kuwa huenda Marekani imekidungua kwa bahati mbaya kifaa chake ambacho hakijajulikana.

Msemaji wa juu wa majeshi ya Iran Abofalzi Shekarchi amesema ndege zake zote zisizo na rubani zimerejea salama kwenye kambi yake, baada ya operesheni zake za utambuzi na udhibiti kwenye maeneo ya Ghuba na lango hilo la Hormuz na hakuna taarifa yoyote ya shambulizi hilo la manowari ya USS Boxer, hii ikiwa ni kulingana na shirika la habari la Tasnim.

Kisa hicho kimeibua wasiwasi wa mzozo wa kikanda unaohusisha Marekani na washirika wake kwenye ukanda wa Ghuba.