1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watawa wa Tibet wafanya maandamano mapya China

15 Machi 2008
https://p.dw.com/p/DOyY

BEIJING:

Watawa wa Kibudha kutoka Tibet wamefanya maandamano mapya katika wilaya ya Gansu,kaskazini-magharibi ya China.Polisi walitumia gesi ya kutoa machozi kuvunja maandamano hayo kwenye nyumba ya watawa ya Labrang, ambayo pia ni hekalu kubwa kabisa ya kibudha nje ya Tibet.

Hapo awali,serikali ya Tibet inayodhibitiwa na China,ilitoa mwito kwa waandamanaji katika mji mkuu wa Tibet-Lhasa kusalim amri kwa polisi hadi Jumatatu usiku ama sivyo watakabiliwa na adhabu kali.Vifaru na magari ya kijeshi yanapiga doria katika mitaa ya Lhasa ili kuzuia watu kutoka nje.Hatua hiyo imechukuliwa baada ya hadi watu 10 kuuawa siku ya Ijumaa katika mapambano yaliyozuka kati ya polisi na waandamanaji.

Lakini ripoti zisizo rasmi zinasema,idadi ya watu waliopoteza maisha yao huenda ikafikia 100.Huu ni uasi mkubwa kabisa wa kisiasa katika kanda hiyo ya Himalaya tangu miaka 20 iliyopita.Machafuko hayo yanatokea wakati China ikijitayarisha kwa Michezo ya Olimpiki itakayofanywa nchini humo katika mwezi wa Agosti.