1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watoto wakimbizi Australia sasa wataka kujiua

Lilian Mtono
27 Agosti 2018

Watoto wa wakimbizi wanaoishi kwenye vituo vya kuhifadhi wahamiaji vya Nauru, vinavyosimamiwa na Australia wanaelezwa kuwa wamekuwa wakijidhuru kwa makusudi na kutafuta mitandaoni jinsi wanavyoweza kujiua.

https://p.dw.com/p/33pPb
Australien Flüchtlinge auf Insel Nauru 2015 Protest
Picha: picture-alliance/dpa/Refugee Action Coalition Sydney

Ufichuzi huu ni kulingana na taarifa zilizotolewa na watumishi wa zamani wa afya, ambao hivi sasa ni watoa taarifa, walipozungumza na kituo cha utangazaji cha Australia, cha ABC.

Nyaraka zilizovuja, zilizokusanywa na wafanyakazi wa uhamiaji , ambazo kituo hicho cha utangazaji cha ABC hatimaye kilizipata zimefichua kile kinachotajwa kama "visa vilivyoongezeka vya kushtusha vya kujidhuru wenyewe" katika vituo vya kuhifadhi wahamiaji vilivyoko kwenye kisiwa hicho cha Nauru, hii ikiwa ni kulingana na taarifa ya habari hii leo.

Kisa kimoja kilichoripotiwa kuanzia mwezi Juni mwaka huu, kilisema mtoto mmoja mkimbizi mwenye miaka 14, alijimwagia mafuta ya petroli na kujichoma moto.

Ripoti nyingine iiyotolewa mwezi huohuo ilionyesha mtoto mkimbizi wa miaka 10 alijaribu kujidhuru mwenyewe kwa kujichoma na vitu vyenye ncha kali, ambavyo vilifanana na vile vilivyopo kwenye waya wa uzio.

Australien schließt umstrittene Asyl-Heime auf Pazifik-Inseln
Kulingana na wafichuzi hao, watoto hawa wamekuwa wakiwaza kufa tu, kutokana na kukata tamaa na mshituko mkubwa.Picha: picture-alliance/dpa/Rural Australians For Refugees

Mtaalamu wa wa zamani wa matatizo ya kisaikolojia kwa watoto kwenye kisiwa hicho aliyeajiriwa na kandarasi ya afya serikali ya Australia, ya International Health and Medical Services, IHMS, kuanzia mwezi Agosti 2016 hadi mwezi Aprili mwaka huu, Vernon Reynolds, amekiambia kituo hicho cha ABC kwamba alikuwa na wasiwasi mkubwa kwamba watoto wanaweza kufa.

Alisema watoto walikuwa wakionyesha dalili za mshituko mbaya sana. Kuna takriban wakimbizi watoto 900 pamoja na waomba hifadhi katika eneo la Nauru, ambao ni pamoja na zaidi ya watoto 120. Kulingana na Umoja wa Mataifa, watoto 40, wamekuwa wakiishi katika eneo hilo katika muda wote wa maisha yao.

Wizara ya mambo ya ndani ya Australia haikupatikana mara moja kuzungumzia ufichuzi huo.

Libyen Tripolis illegale Migranten
Australia wakati huu inafuata sera yake kali ya kuwazuia wahamiaji ambao bado hawajasajiliwaPicha: picture-alliance/Xinhua/H. Turkia

Mfanyakazi mwingine wa huduma za kijamii, Fiona Owens aliyeajiriwa na IHMS kama kiongozi wa timu iliyotoa huduma za afya ya akili kwa watoto kuanzia mwezi Mei mwaka huu, alidai kwamba alishuhudia ongezeko la kutia wasiwasi la visa vya watoto wakimbizi wanaojidhuru wenyewe.

Alikiambia kituo cha ABC kwamba, kitu pekee ambacho watoto wengi wanafikiria kwa sasa ni namna wanavyoweza kufa. Wanatafuta kwenye mtandao wa intaneti wa google.

Australia inafuata sera yake kali ya kuwakataa wahamiaji ambao bado hawajasajiliwa, wanaoingia nchini humo kupitia baharini, na ilianza kutekeleza sheria ya kuwachunguza wahamiaji kabla ya kuingia nchini humo, katika visiwa vya Manus na Nauru vilivyoko kusini mwa Bahari ya Pasifiki kuanzia mwaka 2013.

Mwaka 2016, Australia ilifikia makubaliano na Marekani ya kuwahamisha wakimbizi 1,250 kutoka visiwa vya Nauru na Manus. Lakini kutokana na zuio lililowekwa na rais Donald Trump kuhusu wahamiaji kutoka mataifa saba yanayokaliwa na idadi kubwa ya Waislamu, familia nyingi zinazotokea mataifa hayo, kama Iran na Sudan bado hazijakubaliwa.

Owen amesema, watoto wamekata tamaa kwa sababu wazazi wao tayari wameonyesha hilo, kwa kuwa familia nzima  iliamini kwamba tumaini lao pekee ni kwenda Marekani lakini hivi sasa matumaini hayo yametoweka. 

Mwandishi: Lilian Mtono/DPAE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman