1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 17 wauawa kwa mabomu Pakistan

Kabogo Grace Patricia13 Novemba 2009

Katika mashambulio hayo ya kujitoa mhanga watu wengine zaidi ya 80 wamejeruhiwa.

https://p.dw.com/p/KWPc
Wanajeshi wakiwa katika eneo la Peshawar, Pakistan yalikotokea mashambulio hayo.Picha: AP

Mashambulio mawili ya mabomu ya kujitoa mhanga yaliyokuwa yakizilenga ofisi za idara ya upelelezi na kituo cha polisi kaskazini-magharibi mwa Pakistan, yamewaua watu 17 na yamewajeruhi watu wengine zaidi ya 80.

Mashambulio hayo ya mabomu yaliyokuwa yametegwa kwenye gari yametokea hii leo, wakati jeshi la Pakistan likiripoti kuwa zaidi ya wanajeshi 12 na wanamgambo sita wamekufa katika operesheni inayoendelea katika wilaya ya Waziristan Kusini, wilaya iliyopo katika mkoa huo huo. Mtu alijejitoa mhanga aliliripua gari lake lililokuwa na mabomu karibu na makao makuu ya idara ya upelelezi-ISI huko Peshawar, na kuwaua watu 10 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 60. Shambulio hilo liliharibu sehemu kubwa ya jengo la ofisi hizo za ISI lenye ghorofa tatu. Idara ya uhusiano wa umma katika ofisi za ISI imesema kuwa wafanyakazi saba wa usalama ni miongoni mwa waliouawa huku waliojeruhiwa wakiwa ni raia na wafanyakazi wa ISI.

Mashambulio mengine

Saa moja baadaye gari lililokuwa na mabomu liliripuka karibu na kituo cha polisi cha Bannu, kiasi kilometa 130 kutoka kusini mwa Peshawar na kuharibu vibaya kituo hicho. Mkuu wa polisi wa mkoa huo, Iqbal Marwat amesema askari polisi watano na raia wawili waliuawa na watu wengine zaidi ya 25 walijeruhiwa. Marwat amesema watuhumiwa watatu waliokuwa wanashikiliwa mahabusu pia walijeruhiwa.

Wanamgambo wa Taliban wamewaua zaidi ya watu 300 katika mashambulio ya kujitoa mhanga tangu kati kati ya mwezi uliopita wa Oktoba wakati majeshi ya Pakistan yalipoanzisha operesheni kubwa katika eneo la Waziristan Kusini lililopo karibu na mpaka na Afghanistan. Wilaya ya Waziristan Kusini iliyozungukwa na milima inachukuliwa kama kitovu cha ugaidi duniani, ambako kundi la mtandao wa kigaidi al-Qaeda linapanga na kufanya mashambulizi dhidi ya majeshi wa mataifa ya Magharibi yaliyopo nchini Afghanistan.

Watu waliouawa tangu kuanza operesheni

Maafisa wa Pakistan wamesema mashambulio yanayoongezeka nchini humo dhidi ya maafisa wa usalama na raia, hayataathiri msimamo wa kuendelea na operesheni katika wilaya ya Waziristan Kusini, eneo ambako wanamgambo wanaendelea kusakwa. Kwa mujibu wa taarifa za jeshi la Pakistan, kiasi wanamgambo 522 wameuawa katika operesheni hiyo, huku wanajeshi 51 wakiwa wameuawa. Aidha, katika tukio jingine wanamgambo walivamia msafara wa magari yaliyobeba vifaa kwa ajili ya majeshi ya kigeni nchini Afghanistan katika jimbo la Blochistan lililopo kusini-magharibi mwa Pakistan na kumuua dereva mmoja na kisha kuyateketeza kwa moto malori matano ya mafuta. Junid Arshad, afisa wa ngazi ya juu wa polisi katika jimbo hilo amesema wanamgambo kadhaa walishambulia magari hayo kwa roketi, mabomu ya kutupa kwa mkono na bunduki katika mgahawa mmoja ambako magari hayo yalikuwa yameegeshwa. Arshad amesema dereva mmoja alijaribu kuondoa gari lakini walilishambulia gari hilo kwa risasi na kufanikiwa kumuua na kuwajeruhi watu wengine wawili.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (DPA)

Mhariri: Abdul-Rahman